SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imetenga sh bilioni 1.2 kwa ajili ya kutengeneza miundombinu ya maji, umeme, mahema, uzio pamoja na njia za kupita ikiwa ni maandalizi ya Siku ya Chakula Duniani, itakayoadhimishwa Oktoba 10 hadi 16 Kisiwani Pemba.
Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Shamata Shaame Khamis, amesema hayo alipokuwa akizungumza na HabariLeo kuhusu maadhimisho hayo.
Amesema kiasi hicho cha fedha kimetengwa kwa sababu eneo yatakayofanyika maadhimisho hayo litakuwa ni la kudumu na kwamba Rais Dk Hussein Mwinyi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika siku hiyo.
“Maadhimisho haya yatatoa fursa ya kuelimisha wakulima kuona jitihada na fursa zinazoweza kupatikana katika kilimo,” alisema.
Akizungumzia hali ya lishe visiwani humo, alisema iko imara kwa kuwa mazao mbalimbali yanapatikana sokoni.