WAKALA ya Mbegu za Kilimo (ASA) imeanza kutekeleza agizo la serikali la kuweka miundombinu ya umwagiliaji katika shamba la mbegu la Msimba Kilosa, mkoani Morogoro.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika shamba la Msimba wilayani Kilosa mkoani Morogoro, Mtendaji Mkuu wa ASA, Dk Sophia Kashenge alisema wakala umeanza na hatua za awali za kuchimba visima vya maji vitakavyotumika kufunga mitambo ya umwagiliaji katika mashamba hayo.
Dk Kashenge alisema hadi sasa shamba la Msimba kuna visima vitatu virefu ambavyo vyote vinatoa maji hali ambayo inaonesha dalili njema ya kuwa na maji mengi kwa msimu wote.
Alisema kwa shamba la Msimba ambalo lina zaidi ya hekta 300 zitawekewa miundombinu ya umwagiliaji katika mwaka huu wa fedha hatua itakayosaidia kuongeza uzalishaji wa mbegu kwa msimu mzima wa mwaka.
“Uzalishaji wa mbegu ni kipaumbele chetu, tumepewa maagizo na wizara ya kilimo ya kuhakikisha ndani ya muda mfupi mashamba yetu tuwe tumeweka miundombinu ya umwagiliaji na hili tumekwishalianza kwa hapa Msimba,” alisema.
Dk Kashenge alisema mkakati wa wakala ni kuongeza uzalishaji wa mbegu za alizeti kwa maelekezo ya Wizara ya Kilimo ambapo kwa sasa uzalishaji ni zaidi ya tani 1,000 huku malengo ya mwaka ujao ni tani 5,000 za alizeti katika mashamba yote ya mbegu.
Alisema mashamba yatakayowekewa miundombinu ya umwagiliaji kwa mwaka huu wa fedha ni pamoja na shamba la Msimba wilayani Kilosa Mkoa wa Morogoro, Mwele mkoani Tanga, Ngara Mtoni mkoani Arusha pamoja na shamba la Kilimi mkoani Tabora.
Kashenge alisema hayo ndiyo mashamba ya wakala yatakayoanza kuwekewa miundombinu ya umwagiliaji na baadaye mashamba yote yatawekewa miundombinu hiyo ambapo ni takribani hekta 10,000 zitawekewa umwagiliaji kwa maelekezo ya serikali.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kilosa, Profesa Palamagamba Kabudi alipotembelea shamba hilo alisema wakala wa mbegu umeanza kupiga hatua kubwa za uzalishaji wa mbegu hasa kwa kuanza mifumo ya umwagiliaji.
Alisema mapinduzi makubwa yanafanyika katika sekta ya kilimo hasa ya kuacha kutegemea mvua na kuwa na kilimo cha kisasa cha umwagiliaji.
Profesa Kabudi alisema shamba hilo ni muhimu katika uzalishaji wa mbegu za serikali kutokana na uhitaji wa mbegu nchini.
Alisema bunge limeongeza bajeti kubwa kwa Wizara ya Kilimo hasa katika sekta ya uzalishaji wa mbegu za kilimo. Alisema shamba limekuwa likizalisha mbegu nyingi za alizeti ambazo hupelekwa kwa wananchi tayari kwa kilimo.
Profesa Kabudi alimpongeza Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Mbegu, Dk Sophia Kashenge kwa kuendelea kufanya kazi vizuri na uwajibikaji katika sekta hiyo ya uzalishaji wa mbegu za kilimo.
Alisema hatua ya kuanza kuweka miundombinu ya umwagiliaji katika mashamba ya wakala nchini yataongeza tija ya mbegu kwa wingi na kuifanya nchi iweze kujitegemea na hata kuuza mbegu hizo kwa nchi za jirani.