Mjane arejeshewa kiwanja, nyumba yabomolewa
MWANZA: SERIKALI imeamuru kiwanja kilichopokwa kurejeshwa kwa mjane, Rosemary Cheche, mkazi wa Kata ya Kiseke Wilaya ya Ilemela jijini Mwanza pia utekelezwe ubomoaji wa nyumba iliyojengwa katika kiwanja hicho.
Hatu hiyo imefikiwa baada ya mjane huyo kutoa malalamiko kupitia kliniki ya ardhi Machi 11, 2024 iliyoendeshwa na Naibu Waziri Wizara ya Ardhi, Geofrey Pinda, ambaye baada ya kupokea ufafanuzi wa mgogoro huo kutoka mamlaka husika, akaamuru nyumba kuvunjwa mara moja.
Ufafanuzi ulitolewa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, Kiomoni Kibamba, ambaye wiki iliyopita alihamishiwa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, akathibitisha kuufahamu mgogoro huo na kwamba alishaamuru nyumba ivunjwe, mjane arudishiwe kiwanja chake.
Mwandishi wa habari hii ameshuhudia askari wasaidizi wa Manispaa ya Ilemela wakitekeleza agizo la Naibu Waziri, huku mjane huyo akitoa pongezi kwa serikali kumaliza mgogoro huo uliodumu takribani miaka minane.
“Nashukuru serikali kuniona mimi mjane. Nimetendewa haki bila kujali uwezo wa kifedha wa aliyenivamia, ambaye ni wakili,” amesema.
Mdaiwa, Joseph Mugabe, amefika eneo la tukio na kutaka uvunjaji usimamishwe kwani kiwanja ni chake, na kwamba naye yuko katika harakati za kuonana na Naibu Waziri.
Baada ya muda mfupi aliafiki ubomoaji huo na kuomba kupewa muda wa kusalimisha mali zilizokuwemo ndani, hata hivyo ombi likakubaliwa.