Mjane kukabidhiwa nyumba kesho Chanika

DAR ES SALAAM; MWANAHARAKATI wa masuala ya kijamii, Godlisten Malisa amesema kesho watakabidhi rasmi nyumba ya mjane Judith Ruhumbika iliyojengwa Chanika, Dar es Salaam.

Kupitia ukurasa wake wa instagram, Malisa amesema mjane huyo walimtoa kituo cha mabasi Ubungo, Dar es Salaam akiwa anahangaika na wanaye baada ya mumewe kufariki.

Amesema hakuwa na sehemu ya kukaa wala kwenda na kwamba asubuhi alikuwa anaenda mtaani kuomba kazi za kufua majumbani kwa watu, jioni anarudi kujiegesha na wanaye Ubungo.

“Lakini kwa neema ya Mungu tuliweza kuwatoa pale stendi, tukawapangia makazi ya muda na baadaye kuwajengea nyumba hii ambayo tutaikabidhi jumapili. Ni nyumba ya vyumba vitatu self contained, yenye huduma zote muhimu,” ameandika Malisa na kuongeza:

“Hata hivyo wakati tukijiandaa kwa tendo jema la kukabidhi nyumba, tusisahau tuna mtoto Amina anayepigania maisha yake kitandani pale JKCI. Anahitaji Sh milioni 8 ili aweze kufanyiwa upasuaji. Furaha yetu ya kukabidhi nyumba jumapili itakamilika kama mtoto Amina naye atakua amepata fedha za matibabu,” amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button