MJANE wa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dk John Magufuli, Janeth Magufuli na mjane wa Waziri Mkuu Mstaafu, Rashid Mfaume Kawawa, Asina Kawawa wameishukuru serikali kwa kuwajali.
Walisema hayo Dar es Salaam wakati Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama alipokwenda kuwatembelea kuwapa salamu za Rais Samia.
“Yaani mfikishie salamu, mwambie mama nashukuru sana, Mungu ambariki sana, tupo pamoja, yeye ni Rais wangu na ni kiongozi wangu. Mwambie mama amefurahi sana, asante sana,” alisema Janeth nyumbani kwake.
Mjane wa Kawawa, Asina aliishukuru serikali na akasema inachokifanya kwao kinawasaidia.
Jenista alisema Rais Samia anaendelea kutekeleza azma ya kuhakikisha wajane wa viongozi wanatunzwa na amekuwa akiweka msisitizo kuhakikisha Janeth anapata huduma zote za msingi kutoka serikalini.
Alisema ni azma ya Rais Samia na serikali kuhakikisha inawajali wajane wa viongozi wakuu wa nchi baada ya kazi kubwa waliyofanya ikiwa ni pamoja na kujua maendeleo yao.
“Tutaendelea kusimamia maagizo, maelekezo ambayo tumekuwa tukiyapokea kila siku kutoka kwa viongozi wakuu wakiongozwa na Rais mwenyewe lakini vilevile tutaendelea kuzingatia maoni, ushauri na yale ambayo mnatamani serikali iwafanyie,” alisema Jenista.