Mjapani Geita Gold aagwa

TIMU ya Geita Gold Fc ya mjini Geita imethibitisha kuachana na wachezaji wake watatu raia wa kigeni ikiwemo kiungo mshambuliaji raia wa Japan, Shinobu Sakai baada ya mikataba yao kumalizika.

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Geita Gold FC, Samwel Didda amethibitisha tarifa hizo leo katika mahojiano maalum na HabariLeo kuelezea mipango ya timu hiyo kipindi hiki cha usajili.

Amewataja wachezaji wengine wa kigeni walioachwa ni aliyekuwa mlinda mlango wa timu hiyo, Mc Arthur Arakaza raia wa Burundi pamoja na beki wa kati, Shown Oduro ambaye ni raia wa Ghana.

Ameongeza, pia Geita Gold Fc imekubaliana kutowaongezea mikataba wachezaji wazawa watatu ambao ni beki wa kushoto, Jeremiah Thomas, mshambuliaji Musa Gadi na aliyekuwa nahodha Daniel Lyanga.

“Kwa hiyo ni wachezaji sita ambao tumekubaliana wakatafute changamoto mpya kutokana na mikataba yao kumalizika, lakini wengine wachache sana ndio ambao tutawavunjia mikataba.”

Amesema maamuzi hayo yamefikiwa kutokana na mapendekezo ya ripoti iliyotolewa na benchi la ufundi lililokuwa likiongozwa na aliyekuwa kocha Mkuu wa timu hiyo, Fred Felix Minziro.

“Kuna baadhi ya wachezaji mikataba yao inaendelea, tutaona umuhimu wao kuendelea kulingana na viwango vyao lakini wachezaji kadhaa pia tutaamua kuwanjia mikataba kutokana na viwango vyao.”

Amesema uongozi wa timu ya Geita Gold unatekeleza hilo kwa kuzingatia vipengele vyote vya kisheria na mikataba ili kuepuka mivutano isiyo ya lazima na wachezaji watakaovunjiwa mikataba ama kuachwa na timu hiyo.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button