Mkakati kuongeza uzalishaji mbegu bora waja

WANACHAMA wa Chama cha Taaluma ya Sayansi Kilimo Mazao Tanzania (CROSAT) ,wanakusudia kuweka mkakati endelevu utakaosaidia kuongeza kiwango cha uzalishaji mbegu bora pamoja na matumizi sahihi ya viuatilifu vya mimea ya mazao.

Matumizi ya mbegu hizo ni zile zilizofanyiwa utafiti kuwawezesha wakulima walio wengi kutumia kwa ajili ya kuleta tija katika sekta ya kilimo nchini.

Katibu Mkuu wa Chama hicho, Patrick Ngwediagi, amesema hayo mjini Morogoro wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kufanyika kwa mkutano mkuu wa mwaka wa chama hicho.

Mkutano mkuu huo unaotarajiwa kufanyika Desemba 19 hadi 20, mwaka huu (2023),na mgeni rasmi wa ufunguzi anatarajiwa kuwa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.

Katika mkutano huo watalaam watawasilisha mada mbalimbali ikiwemo ya hali halisi ya uzalishaji wa mbegu bora na kujadi kwa kina namna ya kuongeza kiwango cha uzalishaji wake kwa lengo la kujitosheleza.

“ Kwenye mkutano mkuu huo wataalam watajadili namna ya kuongeza uzalishaji wa mbegu bora , upatikanaji wa mbegu na mifumo inayotumika kuhakikisha tunapata mbegu bora , tutakuja na mkakati na mapendekezo ya kushauri serikali, jamii kuhusu masuala yote yanayowezesha kupata mbegu bora” alisema Ngwediagi.

Katibu Mkuu wa Chama hicho, alisema kwa sasa matumizi ya mbegu bora hapa nchini si makubwa , hivyo lengo la chama hicho ni kuwezesha wakulima walio wengi waweze kutumia mbegu bora zinazotokana na aina bora za mbegu.

Ngwediagi , alisema mkutano mkuu huo pia utajadili namna matumizi bora ya viatilifu baada ya kuonekana hakuna matumizi sahihi ya viatilifu na hivyo kuchangia madhara kwa wakulima wenyewe ikiwa na kutokupata matokeo yanayokusudiwa kwenye uzalishaji.

“ Kwa mfano mkulima anaweza kutumia kiuatilifu ambacho kilikusudiwa kitumike kwa ugonjwa mwingine,au mdudu mwingine naye akatumia kwa ugonjwa usio kusudiwa akifikiri ya kuwa kila kiuatilifu kinatibu mmea na matokeo yake kumletea hasara”alisema Ngwediagi.

Ngwediagi ,alisema matumizi yasiyo sahihi ya viatilifu yanaweza kuleta madhara kwa afya ya walaji nchini na inaweza kuzuiwa kusafirishwa kwa mazao ya kilimo nje ya nchi hasa ikizingatiwa mazao zote ya nafaka yanayopokelewa nje yanafanyiwa vipimo maalumu kabla ya kuingizwa sokoni.

Kwa upande wake Katibu Msaidizi wa Chama hicho, Dk Yasinta Nzogela, alisema kwenye chama hicho, ushiriki wa wanawake ni mkubwa na wamehamasika kujiunga wakitokea kwenye Taasisi za Kitaaluma vikiwemo Vyuo vikuu, Vyuo vya Kati na kuendelea kuhamasisha waliopo katika serikali za mitaa.

Dk Nzogela ,aliwataja wanawake wengine ni kutoka kwenye sekta binafsi wanaomiliki makampuni ya kilimo na mashamba ili na wao waweze kunufuika kwa kupata elimu sahihi , kupata mawazo chanya tofauti katika kuendeleza shughuli zao kilimo.

Mwisho.

Habari Zifananazo

Back to top button