Mkakati waandaliwa kupunguza maambukizi ya VVU

Mkakati waandaliwa kupunguza maambukizi ya VVU

MKUU wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego ameahidi kuja na mkakati wa pamoja utakaosaidia kupunguza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) mkoani humo.

Akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Afya ya Msingi ya mkoa huo, Dendego alisema Mkoa wa Iringa ni wa pili baada ya Mkoa wa Njombe ukiwa na zaidi ya asilimia 11 ya maambukizi ya virusi hivyo.

“Maambukizi haya ni makubwa. Ni muhimu tukaja na mkakati wa pamoja utakaosaidia kukabiliana na janga hili linalotishia zaidi vijana wetu kutokana na mfumo wao wa maisha,” alisema.

Advertisement

Akizungumzia mfumo wa maisha yanayopendwa na vijana, Mkuu wa Mkoa alionya akisema vijana wengi wanaangamizwa na janga hilo kwa kupitia mambo ya hovyo wanayoiga katika mitandao mbalimbali ya kijamii.

“Yanayotazamwa na baadhi ya watoto wetu katika mitandao kupitia simu za mkononi ni mazito kutazamwa hata na wazazi na mambo hayo yanachochea ushawishi unaowatumbukiza kwenye ngono zisizo salama na hatimaye kuangamia,” alisema.

Aliwaomba wazazi kurudi kwenye kazi yao ya msingi ya malezi bora kwa kusema na vijana wao ili wachukue tahadhari na viongozi wa dini kuendelea kuwajenga waumini wao kiimani.

Takwimu za hivi karibuni za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Ukimwi (UNAIDS) zinaonesha maendeleo katika kuzuia VVU na matibabu vinadorora ulimwenguni na kuwaweka mamilioni ya watu katika hatari kubwa.

Kupitia ripoti ya UNAIDS iliyotolewa Julai, mwaka huu katika kongamano la kimataifa la Ukimwi lililofanyika Montreal, Canada inaonesha athari za VVU kijinsia hasa kwa vijana wa kike na wasichana wa kiafrika.

Ripoti hiyo iliyochapishwa katika mitandao mbalimbali inaonesha athari kwa vijana hao zilitokea katikati ya kukatizwa au kupungua kwa huduma za matibabu na kinga za VVU, wasichana walioacha shule kwa sababu mbalimbali, kuongezeka kwa mimba za utotoni na ukatili wa kijinsia.