Mkakati wasaidia kupunguza athari za maafa

MKAKATI wa nchi wa kupunguza athari za maafa (2020-2025) na uwezo wa jamii katika kupunguza na kukabili maafa, umechangia kwa kiwango kikubwa kupunguza athari za maafa nchini hasa zinazosababishwa na shughuli za kibinadamu.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Michael Mmanga, jijini hapa wakati akifungua warsha ya kuandaa taarifa ya nchi ya utekelezaji wa mkakati wa kimataifa wa Sendai (2015-2030).

“Uwepo wa mkakati wa nchi wa upunguzaji wa athari za maafa (2020-2025) na uwezo wa jamii katika kupunguza na kukabili maafa, umeongezeka na hivyo kusaidia kupunguza athari za maafa nchini,” alisema.

Advertisement

Mmanga alisema nchi imekuwa ikishuhudia kuongezeka kwa matukio ya majanga ambayo yamekuwa yakisababishwa na sababu mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi na shughuli za kibinadamu, lakini mkakati huo umesaidia kupunguza athari hizo na hivyo maendeleo yaliyofikiwa kutovurugika.

“Kwa ujumla, majanga haya yamekuwa yakisababisha matokeo hasi katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi kutokana na kupotea kwa mafanikio yaliyopatikana kwa muda mrefu na hivyo kuzorotesha hatua za maendeleo,” alisema.

Naye Mshauri Mkuu Afrika kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupunguza Hatari za Maafa (UNDRR), Hachim Badji aliipongeza serikali kwa kuendelea kuchukua hatua za kukabili maafa pamoja na kushirikisha taasisi mbalimbali.

Kwa upande wake, Ofisa Mwandamizi Uratibu wa Maafa kutoka Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Juvenal Kisanga alibainisha kuwa shirika hilo limekuwa likifanya kazi kwa kushirikiana na serikali kuhakikisha maafa yanadhibitiwa na wananchi kuendelea kufanya shughuli zao.