SINGIDA: Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Moses Machali amewataka wazazi wilayani Mkalama kuhakikisha wanapeleka watoto wao katika vituo vya afya kupatiwa chanjo ya Surua la Rubella ili kuepuka madhara yanayowezajitokeza ikiwa mtoto hatopata huduma hiyo mapema.
Agizo hilo amelitoa wakati wa uzinduzi wa kampeni ya chanjo iliyofanyika katika hospitali ya Wilaya ya Mkalama na kushuhudiwa na wakuu mbalimbali wa Idara, watumishi wa afya pamoja na wananchi walioleta watoto wao kwa ajili ya huduma ya chanjo.
“Chanjo hizi ni safi na salama,kuwa mjanja peleka mwanao akachanjwe, itakuwa jambo la ajabu kutompeleka mtoto wako kupatiwa chanjo.
Viongozi wa serikali wa vijiji hakikisheni mnahamasisha wananchi ili tuweze kufikia lengo lililowekwa na serikali” amesema DC Machali.
Awali akizungumza kuhusu kampeni hiyo ya chanjo, Mganga Mkuu wa Wilaya Dk Solomon Michael amesema kampeni hiyo ya chanjo inatarajia kufikia watoto takribani elfu 34,818 huku akiwataka kila mzazi anamleta mtoto kituo cha afya kupatiwa huduma hiyo.
Tukio hilo litadumu kwa muda wa siku nne likianza jana Februari 15 na litafikia tamati Februari 18 mwaka huu.