Mkali wa Hisabati aliyelibeba taifa

HISABATI ni somo linalochukuliwa na baadhi ya watu kama somo gumu lakini kwa wengine limekuwa somo rahisi, jepesi na linaweza kuleta ushindi kwa mtu anayelipenda na kujifunza kwa dhati.

Hivi karibuni Tanzania imeibuka kidedea baada ya kunyakua ushindi wa tatu katika shindano la hisabati kwa nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki aliyeiwakilisha nchi akitunukiwa medali ya shaba.

Mshindi aliyeiletea heshima taifa katika shindano hilo la hisabati si mwingine bali ni mwanafunzi aliyemaliza kidato cha nne mwaka jana katika Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Feza, Haris Phares. Haris ni mtoto wa pili kati ya watoto watatu katika familia ya Phares Magesa na Haika Lawere, wa kwanza akiwa ni kaka yake Pakston anayesoma kidato cha sita na mdogo wake wa kike.

Akizungumza na HabariLEO Jumapili, Haris anasema amezaliwa Dar es Salaam na kusoma Shule ya mchepuko wa Kiingereza Peninsular kuanzia chekechea hadi darasa la saba. Harris alipohitimu darasa la saba alijiunga na kidato cha kwanza hadi cha nne katika Shule ya Sekondari ya Wavulana Feza na kumaliza mwaka jana.

Akiwazungumzia wazazi wake anasema kuwa baba yake Phares ni mtaalamu wa IT ana kampuni inayoitwa a2zIT ambayo inafanya kazi ndani na nje ya nchi wakati mama yake akiwa ni mmiliki wa hoteli inayojulikana kwa jina la Mbezi Garden. Pamoja na ushindi huo wa Hisabati aliouleta kwa taifa, anasema haikuwa rahisi kwa kuwa alipomaliza darasa la saba alifanya usaili wa kidato cha kwanza ili aweze kujiunga na shule hiyo ya Feza.

Kwa maelezo yake anasema usaili wa kuandika alifanya vizuri isipokuwa wa ana kwa ana hakufanya vizuri. “Usaili wa kuandika nilipita lakini usaili wa ana kwa ana ambao ulikuwa na maswali 12 yaliyokuwa ya logic nikakosa maswali kama 10 kwa hiyo walinikataa… nilivunjika moyo nikawa nalia nikamkimbilia baba, halafu yeye akaomba nipewe nafasi ya pili niweze kufanya huo mtihani tena siku tatu zijazo kuanzia siku hiyo.

“Kwa hiyo nilienda nyumbani tukaa na kaka yangu, tulikaa wote tukaanza kufanya maswali yote na hapo nikaanza kupenda Hisabati, niliporudi kufanya mtihani nilifaulu,” anasema.

Anaelezea somo hilo la Hisabati kuwa ndio kitu pekee ambacho yeye na kaka yake wamekuwa wakishindana, kwa kuwa kaka yake amechukua masomo ya sayansi na yeye biashara, japo kaka yake amemzidi sana kwenye somo hilo. Harris anasema anapenda somo hilo kwa kuwa ni la kutumia maarifa na uelewa zaidi siyo kukariri. “Hisabati inachangamsha bongo, yaani unatumia akili, hauitumii kumbukumbu,” anasema.

Kwa kutambua kuwa anapenda somo la Hisabati wazazi wake wamekuwa wakimsaidia kila anapohitaji msaada wao kwa kuwa yanapotokea mashindano yoyote anapowaomba fedha wanamlipia. “Wakati mwingine ninahitaji kiasi cha Sh 50,000 au 60,000 lakini wakati mwingine ni shilingi 10,000 tu.

Wamekuwa wakinisaidia sana halafu pia wananipa vitendea kazi kama vile simu na intaneti, natumia kuangalia video kwenye YouTube namna ya kujibu maswali, inanisaidia kupanua uwezo wangu,” anasema. Anaeleza mbali na kupata msaada kutoka kwa wazazi na kaka yake, amekuwa akishindana na wanafunzi wenzake kwenye somo hilo kwa kuwa ndilo linalowaunganisha wengi.

Harris anasema walimu nao ni sehemu kubwa katika ufaulu wake wa somo hilo akimtaja mwalimu Seif na Sinde ambao wamemfikisha hapo alipo hata kufikia hatua hiyo ya kimataifa katika ushindani wa somo hilo. Pamoja na kupenda Hisabati hadi kupata ushindi, Harris anaelezea ndoto zake za baadaye angependa kuwa mchoraji wa katuni na uwezo wa kuchora anao.

“Ninaweza kuchora katuni na nimeona kwamba eneo linalohamasisha watoto zaidi ni katuni za vitu mbalimbali. Matarajio yangu nije kuendeleza kipaji changu cha kuchora …nataka kuwa animator,” anasema. Hivi sasa anasema anasubiri kuendelea kidato cha tano na sita katika Shule ya Kimataifa ya Feza na kuwa amepewa ufadhili wa masomo baada ya kupunguziwa asilimia 40 katika ada yao kutokana na kufanya vizuri katika mitihani yake ya kidato cha nne.

“Hiyo imewezesha wazazi wangu wajikaze kidogo niweze kusoma kule maana mazingira ni mazuri na pia mtaala wao unatumia mambo mbalimbali ambayo nimeyapenda… matokeo yangu ya kidato cha nne nilichukua masomo tisa na nilipata A kwenye masomo yote hivyo nilipata daraja la kwanza pointi 7.

“Ninachoweza kusema ni kwamba hizo A tisa hazikuja kirahisi, nilikuwa napata shida sana kwenye somo la Historia na Kiswahili, somo la Historia kwa sababu ilitegemea sana kukariri kitu ambacho sipendagi sana, napenda zaidi mambo ya kuelewa na kama kuhesabu, uwekaji hesabu au account, bookkeeping au hisabati.

Kuna muda kwenye historia nilikuwa napata C lakini nikajitahidi mwishoni nikapata A hata Kiswahili maana nyumbani tunazungumza Kiingereza, mama na baba tunazungumza nao Kiingereza na nilisoma mchepuko wa Kiingereza kuanzia chekechea hadi sasa,” anasema.

Harris anasema somo la Kiswahili sio gumu ila ujibuji maswali yake unahitaji maneno na sarufi sahihi na anaongeza kuwa shida alikuwa anapata kwenye ngeli. “Kuna wakati hata Kiswahili nilikuwa napata D kwa hiyo nikaamua nijikaze mwishoni nikapata A zote,” anasema na anaongeza sababu lugha ya Kiingereza inayotunga mitihani hiyo inakuwa ngumu kuliko mitihani mingine.

“Kuna misamiati mbalimbali inatumika katika swali na usipoelewa swali linataka nini unaweza kukosa jibu kabisa, cha pili walimu shuleni, nimebahatika kusoma shule ambayo ina walimu wazuri wa Hisabati wamenisaidia kujifunza na kuziweza vizuri hesabu,” anasema.

Akizungumzia ushindi alioupata anasema hapa nchini walishiriki wanafunzi sita, watatu walitoka Feza na wawili Shule ya Sekondari ya Mbeya na mmoja Shule ya Sekondari Inspire. “Hisabati sio lazima iwe ngumu kwako mimi naona ukifanya bidii hata kama hauna uwezo kama wengine lakini ukiweza kujua mfumo wa namna ya kujibu maswali mengi itakusaidia kuelewa.

Mimi shuleni kuna wakati ninakuwa nimechoka hivyo natumia muda huo kufanya hisabati ili niweze kujichangamsha,” anasema. Anasema Chama cha Hisabati Tanzania (Chahita) walianzisha mashindano hapa nchini wakafanya mitihani miwili ambayo hao sita ndio waliokuwa sita bora wakaandaliwa kwa ajili ya ushiriki wa shindano hilo la Ukanda wa Afrika Masharika na nchi saba zilishiriki.

Nchi zilizoshiriki ni Tanzania, Rwanda, Kenya, Uganda, Burundi, Ethiopia na Sudan Kusini. Harris anasema alishika nafasi ya tatu na ni Mtanzania pekee aliyepata medali hiyo. Ansema anapopata nafasi yoyote huwa anashiriki katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.

Mama yake Harris Mama mzazi wa Harris, Haika anasema amegundua kipaji cha mtoto wake kuwa anajua hisabati akiwa sekondari na anaongeza kuwa akiwa shule ya msingi alikuwa akifanya vizuri kwa kuwa wa kwanza au wa pili.

“Sababu kubwa ya Harris kupenda hesabu ni Pakston ambaye ni kaka yake yupo kidato cha sita, yeye anapenda sana hesabu na alikuwa anashinda sana hesabu katika shule alizosoma, nilianza kuona pale kipaji,” anasema. Pia anasema amekuwa akiwakuta watoto wake hao wakiwa peke yao likizo wanafanya hisabati kupitia YouTube wakiwa wanashindana, ndipo alipogundua wanapenda hisabati kwa kuwa wengi hawapendi.

“Nawashauri wazazi kama una uwezo kulipa fedha kidogo ukamtafutia mtoto shule nzuri lipa. Lakini hata kama shule zenye shida ya walimu kule kuna masomo ya ziada na wekeza kwenye hesabu kwa sababu uwezo wa mtoto unapanuka,” anasema.

Kwa mujibu wa Haika, elimu ya mtoto ni uwekezaji, mzazi anatakiwa kumsimamia au kuwasimamia na kumfuatilia mtoto asimwache kwa kuwa mtoto hatokei kufaulu tu anajengwa na kutengenezwa.

Aprili 20, mwaka huu ulifanyika mtihani wa mashindano ya hisabati ukanda wa Afrika Mashariki na nchi saba zilishiriki ikiwemo Tanzania. Mitihani hiyo iliratibiwa Rwanda kila mwakilishi wa nchi alifanya mitihani wakati mmoja katika nchi husika, huku kukiwa na uangalizi wa picha kupitia teknolojia ya mikutano ya zoom.

Hayo ni mashindano ya mara ya kwanza katika Ukanda wa Afrika Mashariki hivyo mpango ni kuyaboresha mashindano ya ndani ili kuwawezesha washiriki waweze kushiriki.

Naye Katibu wa MAT, Dk Said Sima anasema mashindano hayo ni tofauti na mitihani ya kawaida inayofanyika ya kidato cha tano na sita hapa nchini kwa kuwa maswali yake yanapima uelewa, kipaji na ufahamu wa mwanafunzi husika. Baba mzazi wa mwanafunzi huyo, Phares Magesa anamshukuru Mungu kwa kumwezesha mtoto wao kuwa mshindi, pia aliwashukuru walimu kwa ushirikiano mkubwa wanaompa Harris pamoja na MAT kwa kushiriki mashindano hayo yanayoonesha vipaji.

“Cha msingi ili mtoto akue vizuri ushirikiano ni muhimu baina ya wazazi, walimu na mtoto mwenyewe,” anasema. Katika mashindano hayo mshindi wa kwanza alipata medali ya dhahabu, mshindi wa pili medali ya fedha na mshindi wa tatu medali ya shaba.

Habari Zifananazo

Back to top button