Mkanda suluhu utokaji damu nyingi baada ya kujifungua
CHANGAMOTO ya wanawake kutoka damu nyingi baada ya kujifungua, imepatiwa suluhu baada ya teknolojia ya mkanda salama kugunduliwa.
Mkanda salama ni teknolojia inayofungwa kwenye kitovu baada ya mwanamke aliyejifungua kupata changamoto ya kutokwa na damu mfululizo, ambao inazuia damu kuendelea kutoka hadi mgonjwa atakapofikishwa kituo cha afya kwa matibabu.
Mbunifu James Kalema kutoka Kampuni ya Afyalead ambaye wamewezeshwa na serikali sh milioni 40 kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) kwa ajili ya kuendeleza ubunifu huo, ameeleza hayo kwa maofisa wa tume hiyo waliomtembelea kuona matokeo chanya ya fedha za serikali zinazotolewa kwa wabunifu na watafiti hapa nchini.
Amesema ubunifu huo umeleta matokeo chanya kwa asilimia 80 baada ya kufanyiwa utafiti kwa wanawake 120 katika hospitali ya St Francis iliyopo Morogoro.
Kalema amesema wamefanya ubunifu huo kwa lengo la kupunguza vifo vinavyotokana na utokaji wa damu nyingi kwa wanawake nchini baada ya kujifungua.
“Tulipata ufadhili Costech, wa sh milioni 40 baada ya kushiriki Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (Makisatu), na kuwa katika bunifu bora tatu.
“Ufadhili huo umetuwezesha kuongeza ubora wa kifaa chetu, kutuunganisha na wadau mbalimbali lakini pia kusajili kampuni na kupatiwa msaada wa kibiashara namna gani tunaweza tukafanya,” amesema.
Amesema mkanda huo unatumika kumfunga mama kwenye kitovu ili kuzuia damu isitoke, ambapo katika maeneo mengi ya vijijini hutumia njia ya kienyeji ya kumfunga mama kitenge tumboni kwa nguvu kuzuia damu isitoke kwa wingi ili kumuwahisha hospitalini.
Ametaja mikoa inayoongoza kwa tatizo hilo kuwa ni Shinyanga, Mara, Lindi na Mtwara.
Muuguzi katika Hospitali hiyo ya St Francis, Enos Sama amekiri kuwa teknolojia hiyo ya mkanda salama inafanya vizuri kwa wagonjwa walioitumia.
Naye Meneja Uhifadhi Taarifa na Machapisho Costech, Dk Philbert Luhunga amesema tume hiyo inalenga kuonyesha fedha zinazotolewa na serikali kupitia tume hiyo zinavyotoa matokeo chanya kwa jamii.