Mkandarasi akabidhiwa ujenzi bwawa

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule,

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amemkabidhi mkandarasi aliyeshinda zabuni mradi wa ujenzi wa bwawa litakalotumika kwa kilimo cha umwagiliaji katika Kijiji cha Chunyu, Wilaya ya Mpwapwa.

Kampuni ya GNMS Contractors Co. Ltd chini ya Emmanuel Mponda, ambaye ni ya mzawa, ndiyo iliyokabidhiwa.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara, Senyamule aliwataka wananchi kulinda mazingira hasa ya bwawa hilo lenye faida nyingi kwao.

Advertisement

“Bwawa hili litakapokamilika litakuwa na faida nyingi kiuchumi kwa ninyi wakazi wa hapa kwani mtaweza kufanya kilimo cha kisasa pamoja na biashara na kujiongezea kipato,” alisema.

Mkuu huyo wa mkoa alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa Sh bilioni 27 kwa ajili ya ujenzi huo.

Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Josephat Maganga, alionya watakaobainika kufanya uharibifu wa mazingira kwa namna yoyote ile.

Mbunge wa Mpwapwa, George Malima alisema kutokana na Sh bilioni 27 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo, hali ya uchumi wa wakazi wa Chunyu na majirani zao itabadilika.

Ujenzi wa Bwawa la Msagati ulianza kufanyiwa utafiti miaka 10 iliyopita na ujenzi wake unatarajiwa kuanza karibuni baada ya makabidhiano hayo rasmi. Utatumia kipindi cha miezi 18 mpaka kukamilika.

Bwawa linatarajiwa kutumia eneo la ukubwa wa hekta 3,500, litabeba ujazo wa lita trilioni 90 za maji na maji hayo yanatarajiwa kutumika kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji kwa mwaka mzima, kunyweshea mifugo pamoja na matumizi ya kawaida ya nyumbani isipokuwa kunywa.