Mkandarasi akatwa Sh milioni 327 uzembe kazini
DAR ES SALAAM :MKANDARASI anayejenga mradi wa ujenzi wa vyoo vya umma Jijini Dar es Salaam wenye thamani ya Sh bilioni 3.27 unaosimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) , amekatwa zaidi ya Sh milioni 327 kama faini ya kuchelewesha kazi.
Hayo yameelezwa Januari 31,2024 na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU) Mkoa wa Ilala jijini Dar es Salaam, Sosthenes Kibwengo wakati akitoa taarifa ya utendaji wa taasisi hiyo kwa kipindi cha Oktoba na Desemba 2023.
Kibwengo amesema taarifa iiyotolewa katika siku za nyuma na taasisi hiyo kuhusu ukaguzi wa mradi huo, ilibaini kasoro kadhaa ikiwemo kuchelewa kwa kukamilika kwa mradi huo kinyume na mkataba, na kuwataka wakandarasi mkoani humo kukamilisha miradi wanayopewa ndani ya wakati ili kupunguza gharama.
- Aidha, Kibwengo amesema TAKUKURU Ilala imeendelea kutumia mbinu mpya za uelemishaji umma ikiwemo kuendesha mafunzo maalumu kwa walimu walezi 239 wa klabu za wapinga rushwa na kuendesha shindano la ujumbe mfupi kwa wanachama wa klabu hizo huku akisisitiza kuwa kiwango cha uelimishaji kimeongezeka kwa zaidi ya asililimia 300.