Mkandarasi apewa miezi miwili barabara Kidatu-Ifakara

WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ametoa miezi miwili kwa Mkandarasi wa Kampuni ya M/s Reynolds Construction Company kukamilisha ujenzi wa Barabara ya Mikumi-Kidatu-Ifakara, sehemu ya Kidatu-Ifakara yenye urefu wa kilometa 66.9 kwa kiwango cha lami na daraja la Mto Ruaha Mkuu, vinginevyo hatapewa kazi nyingine za ukandarasi .

Bashungwa alitoa maagizo hayo Kidatu wilayani Kilombero mkoani Morogoro baada ya kukagua ujenzi wa barabara hiyo na daraja la Mto Ruaha Mkuu na kutoridhishwa na kasi ya ujenzi ambapo mkandarasi yupo nje ya muda wa mkataba wa kukamilisha mradi huo

“Sijaridhishwa na kasi ya mkandarasi, hivyo ninakupa miezi miwili uwe umekamilisha hii barabara na daraja usupofanya hivyo ukija kuomba kazi yoyote ndani ya nchi hii hatuwezi kumpatia”. alisema Bashungwa.

Licha ya kutoa miezi miwili hadi Aprili 30, mwaka huu, Waziri Bashungwa alisema hataki kuona muda aliopoteza kwa kisingizio cha mvua anawasilisha madai ya yoyote serikalini ya kulipwa kwa kuwa kipengele hicho hakimo kwenye mkataba .

Waziri alisema mkandarasi huyo ameshalipwa fedha zote za kutekeleza mradi huo likiwemo la ujenzi wa daraja hilo kubwa linajengwa kwa viwango imara na ujenzi wa barabara zake.

“Nimemwambia anikabidhi kipande hiki cha barabara na daraja hili Aprili 30, mwaka huu (2024) na gharama za kupoteza muda asituletee sisi serikali kwa sababu alipoingia mkataba na sisi alijua kuna miezi ya kiagazi na mvua hawezi kusingizia mvua” alisema Bashungwa mbele ya mkutanao wake na wananchi wa Kilosa na Kilombero.

Waziri Bashungwa alimtaka mkandarasi hiyo kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kipande hicho cha barabara na daraja hilo kulingana na muda alipewa wa nyongeza.

Waziri Bashungwa alisema barabara hiyo ni kipaumbele cha serikali na Rais Samia Suluhu Hassan, anataka barabara hiyo iwe barabara ya kitaifa kwani inaunganisha mkoa wa Tanga-Morogoro-Njombe pamoja na nyanda za juu kusini hadi kufika Bandari ya Mtwara.

Bashungwa alisema kipaumbele cha barabara hiyo ni kuanzia Bandari ya Tanga – Handeni kwenda Turiani – Kilosa -Mikumi kupita Kidatu – Kilombero kwenda Ifakara -Mlimba kuelekea Lupembe mkoani Njombe hadi Kibena inaunganishwa kwa kiwango cha lami.

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Morogoro, Mhandisi Alinanuswe Kyamba alisema ujenzi wa barabara hiyo unafadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo wa Nchi za Ulaya, ukishirikiana na Shirika la Msaada la Uingereza ( UKAID) pamoja na Shirika la Kimarekani la Maendeleo ya Kimataifa ( USAID).

Mhandisi Kyamba alisema maendeleo ya mradi huo umefikia asilimia 86 ikiwemo ujenzi wa daraja kubwa la Ruaha Mkuu lenye urefu wa mita 133 na madaraja mengine manane na makaravati makubwa 45 na ya kawaida 249.

Alisema muda wa kwanza wa ukamilishaji wa mradi huo ulikuwa Aprili 30, 2020 , lakini ukaongezwa tena hadi Machi 31, 2024 ili kufikia asilimia 100 ya mradi huo .

Mhandisi Kyamba alisema ,pamoja na kuongezewa muda wa nyonyeza, mkandarasi bado yupo nyuma kwa miezi miwili kutokana kutokana na changamoto kadhaa za kiufundi.

Habari Zifananazo

Back to top button