Mkandarasi atakiwa akabidhi mradi wa maji Karagwe

MKUU wa Wilaya ya Karagwe, Julius Laizer amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji wa Ihembe kukabidhi mradi huo kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA),  ili mradi huo utoe huduma haraka kwa wananchi.

Mkuu huyo wa wilaya alitembelea mradi wa maji wa Ihembe wenye thamani ya Sh Milioni 800 unaotekelezwa mkandarasi wa SAJAC Investment, ambaye alipaswa kukabidhi tangu Agosti 30 2022, lakini hakufanya hivyo na ameacha msimamizi wake ambaye hatoi majibu ya kueleweka kwa wananchi na viongozi wa eneo hilo kuhusu mradi.

Alisema RUWASA , pamoja na wanakijiji wa Ihembe wanasubiri mradi huo ukabidhiwe, lakini mkandarasi hajatoa sababu zozote msingi za kutoonekana eneo la mradi, wala sababu ya kutokabidhi mradi huo, kwani inaonekana hatua zote zimekamilika.

“Nimesikitika sana kama mkandarasi anaacha msimamizi ambaye hawezi kujibu maswali yetu, wakati inaonekana mradi upo hatua nzuri, sasa wananchi hawapati haki yao kisa mkandarasi ameamua kutokuja.

“Naomba mkandarasi afike haraka  Karagwe, Kama hawezi kufika serikali itamsaidia kufika, wananchi  wanataka maji  yeye ameshindwa kufika kukabidhi mradi, hatutawavumilia wakandarasi wa namna hii ,” alisema Laizer.

Kaimu Meneja wa RUWASA wilayani Karagwe, Justo Mutabuzi alisema kuwa mradi huo umekamilika kwa asilimia 98  na mkandarasi huyo amekuwa akiandikiwa barua za kufika eneo la mradi  tangu Desemba mwaka jana, ili  kufanya makabidhiano,  lakini bado hajaonekana.

Alisema mradi utahudumia wananchi 3,630 na tayari RUWASA imetoa elimu kwa chombo cha watumia maji katika kijiji hicho,na mkandarasi amelipwa asilimia 75 ya kazi zake, hivyo wanasubiri wakabidhiwe, ili wananchi waendeshe mradi wao wa maji kwa uhuru.

Diwani wa Kata Ihembe, Regina Festo alisema mradi huo una umuhimu mkubwa katika kijiji hicho kutokana na vyanzo vilivyoko kukauka.

Mkuu wa Wilaya pia alitembelea mradi wa maji taka wa Omurushaka Karagwe, ambapo aliwataka kuongeza bidii ya kumsimamia mkandarasi,  ili akamilishe mradi huo kabla ya Machi 30, mwaka huu.

Habari Zifananazo

Back to top button