MKANDARASI wa shule mpya ya sekondari ya wasichana ya Kagera River, amekamatwa kutokana na kusuasua kwa ujenzi.
Hatua ya kukamatwa mkandarasi huyo imekuja, ikiwa ni wili mbili tangu Mkuu wa Mkoa Kagera, Albert Chalamila kufanya ziara ya kujitambulisha na kuagiza mkandarasi huyo Kampuni ya Sre Civil and Building Contractor Limited kuongeza kasi ya ujenzi wa shule hiyo.
Akizungumza katika mradi huo, Chalamila amesema kuwa katika uongozi wake hatakubali kuona miradi inayotekelezwa ndani ya Mkoa wa Kagera ikisuasua au kutotekelezwa kwa wakati, huku tayari fedha zipo.
“Kwa ujumla mradi unakwenda taratibu sana na mkandarasi ningekutafuta kwa mbinu zangu binafsi ingekuwa tofauti, huu si utaratibu, unaitwa wiki mbili hauji.
“Nataka wakandarasi wote mnaotekeleza miradi ndani ya mkoa huu mbadilike na mtekeleze miradi kwa ufanisi, kasi na viwango,” alisema Chalamila.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, Toba Nguvila, alisema kuwa wakati wa ziara ya utambulisho ilielekezwa mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi na kujenga usiku na mchana, jambo ambalo halijafanyiwa kazi na ujenzi bado hauridhishi.