Mkandarasi kikaangoni, RC atoa maelekezo

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima amempa wiki nne msimamizi wa Kampuni ya ujenzi ya Inter Country Contractors, Emmanuel Buzanza kuhakikisha anakamilisha ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa mbili mjini Nansio.

Malima alitoa agizo hilo Jumatano mjini hapa wakati wa ziara ya kikazi ya siku moja, ambayo alipokea malalamiko kutoka kwa wananchi na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ukerewe, Ally Mambina kuwa barabara hiyo imechukua muda mrefu bila kukamilika.

Pia aliuagiza uongozi wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) wilaya na mkoa kuhakikisha wanamfuatilia mkandarasi huyo kwenye eneo la mradi wa barabara hiyo inayojengwa kwa gharama ya Sh milioni 993.

“Nikirudi hapa Oktoba 15 nikute ujenzi umekamilika, tofauti na hapo nyie Tarura na mkandarasi mtawajibika,” alisema.

Awali Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ukerewe, Ally Mambina alisema mkandarasi anayejenga barabara hiyo iliyoko mjini Nansio ameshindwa kukamilisha kazi ya ujenzi wa barabara hiyo na amekuwa akionekana kwenye eneo la ujenzi baada ya kuwepo kwa ziara za viongozi na matukio mengine ya kitaifa.

“Huyu mkandarasi ni muongo na ameshindwa kazi, ameonekana leo hapa baada ya ujio wako na mradi huu uko nje ya muda uliotakiwa kukamilika,” alisema Mambina.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, alisema changamoto inayoikabili wilaya hiyo ni kushindwa kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya vumbi yenye urefu wa kilometa mbili kwa gharama ya Sh milioni 970. Alimwomba mkuu wa mkoa kuitafutia ufumbuzi wake.

Alisema changamoto nyingine ni kushindwa kukamilika kwa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Nansio inayojengwa kwa gharama ya Sh bilioni 11.9 baada ya baraza la madiwani na viongozi wa chama kutokubaliana na gharama za ujenzi.

Mshauri elekezi wa ujenzi wa mradi huo kutoka Kampuni ya Mekon Arch Consult Limited Arch, Stephen Kanda alisema mradi huo ulioanza kujengwa Mei Mosi mwaka huu kupitia Kampuni ya Ujenzi ya Suma JKT umeshindwa kutekelezwa  kutokana na ucheleweshaji wa malipo ya mkandarasi.

Hatua ya kwanza ya ujenzi itahusisha ujenzi wa majengo ya famasi, kuhifadhi maiti, jengo la mama na mtoto na wagonjwa wa nje kwa gharama ya Sh bilioni 2.7 na serikali imetenga Sh bilioni moja kwa ujenzi wa majengo ya hatua ya pili.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button