“Mkandarasi sitarajii maombi nyongeza ya muda”
MTENDAJI Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor Seff amemtaka mkandarasi ‘Salum Motors Transport Co.Ltd’ kukamilisha kwa wakati ujenzi wa barabara ya Kasulu- Kabanga – Kasumo- Muyama Km 36 ambapo awamu ya kwanza ya Km 12.5 inaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami.
Akiwa katika ukaguzi wa barabara hiyo, Mhandisi Seff ameeleza kuwa maagizo yaliyotolewa kwa mkandarasi hapo awali yamefanyiwa kazi kwa kiasi kikubwa na kwamba hatarajii suala la maombi nyongeza ya muda.
“Leo nimekagua barabara hii kwa mkataba huu wa awamu ya kwanza Km 12.5, kazi inaendelea na mkandarasi anatakiwa kumaliza kazi hii ndani ya muda uliopangwa, kwa maana hiyo sitarajii kuona maombi ya nyongeza ya muda kwani hakuna sababu yoyote ya kufanya hivyo”, amesema mhandisi Seff.
Kwa upande wa Naomi Kiogoma mkazi wa kijiji cha Kasumo amesema ujenzi wa barabara hiyo ni mkombozi kwa wakazi wa vijiji hivyo kwani barabara ikikamilika wananchi wataweza kusafirisha mazao kwa urahisi kwenda Kasulu.
“Barabara hii itatusaidia hasa kukuza uchumi wetu, sisi akina mama sasa tutaweza kufanya biashara maana hata kama mtu anataka kuuza mazao kama maharage itakua rahisi kuyafikisha Kasulu.” amesema Naomi.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 36 inajengwa kwa awamu ya kwanza kilomita 12.
5 kwa kiwango cha lami na inatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 18 ambapo itagharimu Sh bilioni 16.7