Mkataba bandari haujakiuka Katiba
MAHAKAMA imeeleza kuwa mkataba wa IGA kuhusu uwekezaji wa bandari haukukiuka vifungu vya Katiba au sheria mbalimbali za nchi.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Jaji Projestus Kahyoza amesema katika taarifa yake kwa wanahabari kuhusu hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya kuhusiana na kesi ya kupinga uwekezaji wa mkataba wa bandari kati ya Tanzania na Dubai.
“Leo tarehe 10 Agosti, 2023, jopo la majaji wa Mahakama Kuu, Masjala Kuu liliketi na kutoa hukumu kuhusiana na kesi iliyofunguliwa na waombaji wanne, Alphonce Lusako, Emmanuel Kalikenya Chengula, Raphael Japhet Ngonde na Frank John Nyalus.
“Malalamiko hayo waliyawasilisha kama kesi ya kikatiba na yaliwasilishwa dhidi ya mwanasheria mkuu wa serikali, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Katibu wa Bunge,” imesema taarifa hiyo.
“Katika hukumu yake, Mahakama imebaini na kuhitimisha kuwa mkataba wa IGA haukukiuka vifungu vya katiba au sheria mbalimbali zilizonukuliwa.
“Aidha Mahakama imetupilia mbali hoja za upande wa waleta maombi kwamba Mkataba wa IGA ulipoka uhuru wa Tanzania kumiliki na kutumia rasilimali asilia bila kuingiliwa na nchi yoyote.
“Vilevile mahakama haikuona kama usalama wa nchi ulikuwa hatarini kutokana na kusainiwa kwa mkataba wa IGA.
“Kwa msingi huo, Mahakama imetupilia mbali shauri hilo na kuamuru kuwa kila upande ubebe gharama zake,” amesema Jaji Kahyoza. Kesi hiyo ilitajwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Julai 3, 2023 na ikaanza kusikilizwa Julai 20, mwaka huu.