Mkataba Mchuchuma, Liganga kaa la moto

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira imelieleza Bunge kuwa hakuna kazi yoyote inayoendelea kwa mujibu wa Mkataba uliosainiwa katika mradi unganishi wa Chuma cha Liganga na Makaa ya Mawe ya Mchuchuma.

Akiwasilisha taarifa ya Kamati leo Februari Mosi, 2023 Mwenyekiti wa kamati hiyo, David Kihenzile amesema licha  ya kusainiwa mikataba katika miradi hiyo lakini inasikitika hakuna kilichofanyika kutokana na sababu za mwekezaji kuhitaji  vivutio vya ziada vinavyolenga kumnufaisha zaidi kuliko maslahi ya Taifa letu.

Amesema vivutio vilivyoombwa na Mwekezaji vilikuwa vikikinzana na sheria mbalimbali za nchini.  Sheria hizo ni pamoja na Sheria za Kodi, Sheria ya Madini, Sheria ya Rasilimali na Maliasili za Nchi.

Amesema, pia ilibaiinika kuwa Mkataba na Mwekezaji huyo una vipengele kadhaa vyenye mapungufu ambayo yanakinzana na maslahi ya Taifa;

Pia, kucheleweshwa na kuongezeka kwa fidia ya wananchi kutoka Shilingi 11,037,183,020.78 kwa uthamini wa mwaka 2015 hadi Shilingi 15,979,788,649.50 mwaka 2022.

Kihenzile amesema,  kiasi hicho kinajumuisha riba itokanayo na kucheleweshwa kwa fidia katika kipindi husika; wakati serikali ikijielekeza katika jitihada za kutafuta mwekezaji mwingine wa kuendeleza mradi, mwekezaji wa awali (SHG) amejitokeza tena na kudai kuwa yupo na ana uwezo wa kutekeleza mradi huo.

“Kuchelewa kwa utekelezaji wa miradi hii takriban miaka 13 kunachelewesha kasi ya maendeleo ya ujenzi wa Viwanda Mama, kushindwa kuongeza thamani ya malighafi za ndani lakini pia kuwakosesha ajira wananchi na kuliingizia Taifa hasara kubwa.”Amesema

Akifafanua suala hilo, Kihenzile amesema mwaka 2011 yalijitokeza Makampuni 48 kutoka nchi mbalimbali duniani kuja kuwekeza katika mradi huo ambapo Kampuni ya Sichuan Hongda Group Corporation (SHG) ilionesha kuwa na teknolojia inayohitajika hususan katika Mradi wa Chuma cha Liganga na kusaini mkataba wa ubia na serikali kupitia shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) t21Septemba 21, 2011 na kuanzisha Kampuni ya Ubia iliyojulikana kama Tanzania China International Mineral Resources Limited (TCIMRL).

Amesema, serikali kupitia NDC inamiliki asilimia 20 na SHG asilimia 80.

“Kamati ilielezwa kuwa asilimia 20 za hisa zinazomilikiwa na Serikali zilipatikana kupitia utaratibu wa ‘Free Carried Interest’ hivyo Serikali haiwajibiki kuwekeza fedha taslim ndani ya mradi ili kumiliki hisa hizo

Amesema, Kamati pia ilielezwa kuwa kwa mujibu wa mkataba uliosainiwa, miradi hiyo unganishi ina vipengere vitano ambayo ni mgodi wa Chuma wa Liganga wenye uwezo wa kuzalisha Tani Milioni 2.9 kwa mwaka; Kiwanda cha kuzalisha bidhaa za Chuma Liganga chenye uwezo wa kuzalisha Tani Milioni 1.1 kwa mwaka; Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Mchuchuma wenye uwezo wa kuzalisha Tani Milioni tatu kwa mwaka;  Kituo cha Kufua Umeme huko Mchuchuma cha Megawati 600 na Msongo wa Umeme wa Kilovoti 220 kati ya Mchuchuma na Liganga na  Barabara kutoka Mchuchuma hadi Liganga (shortcut route).

Amesema, kulingana na makadirio ya mwekezaji, uwekezaji katika mradi huo unganishi utakuwa Dola za Marekani Bilioni 3.0, ambapo mtaji wa mwekezaji ni kiasi kisichozidi Dola za Marekani Milioni 600 na mkopo utakuwa Dola za Marekani Bilioni 2.4.

“Kamati ilielezwa kwamba baada ya kusaini mkataba, Kamapuni ya Ubia ilikamilisha hatua za muhimu ili kuanza ujenzi. Hatua hizo ni Uchorongaji na Upembuzi yakinifu, Upatikanaji wa Leseni Maalum za Uchimbaji wa Mkaa ya Mawe ya Mchuchuma na Chuma cha Liganga kutoka Wizara ya Nishati na Madini wakati huo tangu Oktoba 9, 2014.

Pia, utafiti wa athari za mazingira zitakazotokana na utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na njia za kupunguza athari hizo zilifanyika na kupata vyeti vya mazingira vya Mgodi wa Chuma, Kiwanda cha Chuma, Mgodi wa Makaa ya Mawe Mchuchuma, Kituo cha Kufua Umeme Mchuchuma, na Msongo wa Umeme Kilovoti 220 (Mchuchuma – Liganga).

Amesema vile vile Kampuni imekwishapata vibali vya kutumia Maji  kutoka Mito ya Katewaka, Mchuchuma na Lupali.

“Pamoja na hatua hizo inasikitisha kuona kwamba miradi hii hadi taarifa hii inaporipotiwa hakuna kazi yoyote inayoendelea kwa mujibu wa Mkataba uliosainiwa.”Alisisitiza.

 

Habari Zifananazo

Back to top button