Mkataba wa bandari unaweza kuletwa bungeni-Profesa Kitila

MIKATABA ya uwekezaji inayosainiwa nchini inaweza kuitishwa bungeni kwa marekebisho na maboresho, imeelezwa. Hayo yalibainishwa wakati wa mjadala wa kitaifa wa kulinda na kuendeleza umoja wa kitaifa wakati wa mageuzi ya kisiasa na kiuchumi ulioandaliwa na Kampuni ya Media Brains (MB) Dar es Salaam jana.

Akizungumza katika mjadala huo, Mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo alisema Sheria ya Ulinzi wa Rasilimali za Taifa inaipa mamlaka bunge la kuitisha mikataba iliyosainiwa, hivyo hata mikataba itakayoingiwa kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) na Kampuni ya DPW ya Dubai kama itakuwa na dosari nayo itafikishwa bungeni kwa maboresho.

Pia alisema Kifungu cha 22 cha makubaliano yaliyoingiwa kati ya serikali hizo mbili kinaruhusu kufanyika kwa marekebisho kwenye makubaliano hayo. Kutokana na hilo, alisema Tanzania imechagua kufuata mfumo wa uzalendo wa kiuchumi ambao unatoa fursa kwa mwekezaji yeyote awe Mwarabu, Mzungu au Mwafrika kuwekeza kwa tija kwenye eneo husika.

Advertisement

Pia alisema kampuni hiyo ya Dubai haipewi bandari yote ya Dar es Salaam bali ni maeneo saba tu zikiwamo gati. Mfanyabiashara Rostam Azizi alisikitishwa na mjadala unaoendelea kuhusu bandari kutaka kuwagawa Watanzania kwa misingi ya udini, ukabila na ukanda.

Alisema Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume walifanya kazi kubwa ya kujenga nchi hii katika misingi ya umoja, mshikamano, amani na utulivu. Kuhusu suala la bandari, alisema kama nchi ilishakubaliwa kuwa serikali iondoke katika kufanya biashara na sekta binafsi ichukue nafasi hiyo, hivyo mpango huo wa serikali na Dubai utaleta tija na ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta binafsi (TPSF), Angela Ngalula alisema ana miaka 20 katika shughuli za usafirshaji zinazohusisha matumizi ya bandari, hivyo mpango huo wa serikali utaleta tija maradufu katika bandari hiyo.

Katibu Mkuu wa TEC, Padri Dk Charles Kitima alitaka suala la uwekezaji likiwemo la bandari, sekta binafsi ya Tanzania ndiyo ipewe kipaumbele. Mwanahabari nguli nchini, Jenerali Ulimwengu pamoja na mambo mengine alisema masuala makubwa yanayohusu nchi likiwamo la bandari yafanyike kwa uwazi na ukweli.

Mwanasiasa mkongwe, Stephen Wasira aliwahakikishia Watanzania kuwa bandari wala sehemu yoyote ya Tanzania haiwezi kuuzwa. Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alisema badala ya kuipa DP World kuendeleza na kuendesha bandari, ni vyema serikali ikaunda kampuni itakayoendeleza na kuendesha bandari hizo kwa ubia.