BENKI ya Biashara (NBC) imezindua kampeni ya ‘Mkeka wa Ushindi na ATM za NBC’ itakayowawezesha wateja wake kutwaa zawadi mbalimbali ikiwemo kupata tiketi ya kushuhudia mechi ya Ligi Kuu Bara.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika katika jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Mkuu wa kitengo cha masoko wa NBC, David Raymond, alisema kampeni hiyo imelenga kuhamasisha wateja wa NBC na wasio wateja wa NBC kutumia mashine za ATM za NBC kufanya miamala yao.
Wateja ambao watatumia kadi zao za ATM kufanya miamala mbalimbali katika kipindi cha kampeni watapata nafasi ya kushinda zawadi za kusisimua, ikiwa ni pamoja na tiketi za kushuhudia Ligi ya Mabingwa ya NBC, jezi, na zawadi nyingine kemkem.
Ameeleza kupitia kampeni hiyo, wateja wote wa ATM za NBC hata kama si wateja wa benki hiyo wana nafasi ya kujinyakulia zawadi mbalimbali.
“Tunaelewa umuhimu wa urahisi katika huduma za benki, tunazidi kusogeza huduma za kibenki karibu zaidi na wateja kwa kuongeza ATM mpya kwenye maeneo mbali mbali nchini.
“Watumiaji wa ATM za NBC wanaweza kuweka pesa kwenye akaunti yoyote ya NBC kupitia ATM zilizopo kwenye matawi yetu nchi nzima,” ameeleza Raymond na kuongeza:
“Wale wasiokuwa na akaunti yoyote wanaotumiwa fedha kwa kutumia huduma ya NBC Cash Popote, wanaweza kutoa pesa hizo kwenye ATM yoyote ya NBC. Wote walio na kadi za VISA, Union Pay na Mastercard wanaweza kutumia ATM za NBC kutoa pesa.
“Makundi yote haya yanayo nafasi sawa ya kujishindia Zawadi hizi katika kampeni hii. Tunaamini kuwa watumiaji wa ATM za NBC wataendelea kufurahia huduma zetu, tunawakaribisha wote watumie ATM za NBC.”
Naye Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Kidijitali wa Benki ya NBC, Ulrik Tobias aliongeza kuwa zawadi hizo zitakuwa ni za papo kwa papo, pale mteja akifanya muamala wake kwa kutumia ATM ya NBC atapata kujua kuwa ameshinda zawadi gani kwa kuangalia nyuma ya risiti ya muamala wake.
“Sisi kama benki ya NBC, daima tunawaweka wateja wetu karibu na kuhakikisha wanafurahia huduma zetu wakati wowote na popote. Tunafurahi kuwapa wateja wetu nafasi ya kushinda tiketi za kuona Ligi ya Mabingwa, jezi, na vitu vingine vya kumbukumbu ya Ligi ya NBC. Tunatumaini kuwa kampeni hii itaimarisha zaidi uhusiano wetu na wateja wetu pamoja na watumiaji wote wa ATM zetu,” aliisema.
Kampeni hii inawalenga watumiaji wote wa ATM za Benki ya NBC za Dar es Salaam na Kibaha.