Mkenda afanya mazungumzo na benki ya dunia

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa, Adolf Mkenda leo Machi 23, 2023 amekutana na Mkurugenzi wa Mkazi wa Benki ya Dunia Nathan Belete Jijini Dodoma na kuzungumza mambo mbalimbali kuhusu sekta ya elimu.

Waziri wa Elimu ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuendelea kusaidia sekta ya elimu ambapo amesema kwa sasa wizara ipo katika kufanya mageuzi makubwa ya kielimu kwa kufanya mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na mabadiliko ya Mitaala ili kuwezesha kutoa elimu ujuzi.

Prof. Mkenda ameeleza kuwa serikali inaendelea kuwekeza katika sekta elimu kwa kuwa inatambua uwekezaji katika sekta hiyo utaendelea kunufaisha vizazi hadi vizazi, na kuongeza kuwa mabadiliko yanayotarajiwa kufanyika yanahitaji uwekezaji wa kutosha.

“Mabadiliko haya yanalenga kuwawezesha vijana kuweza kuyamudu mazingira yanayowazunguka pamoja na kuwa na ujuzi utakaowasaidia kujiajiri ama kuajiriwa ili waweze kushiriki katika kukuza uchumi wa chini” amelezea Waziri huyo.

Aidha, Katibu Mkuu  wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Carolyne Nombo ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuendelea kufadhili miradi katika sekta ya elimu ambapo ameitaja baadhi ya miradi kuwa ni BOOST, HEET, ESPJ na SEQUIP ambayo imesaidia kwa kiwango kikubwa katika kuboresha sekta ya elimu

Habari Zifananazo

Back to top button