Mkopo wa nanasi mbili ulivyomuwezesha kumiliki nyumba 2

MICHAEL Elias (44) mkazi wa Mtaa wa Munangi, Kata ya Kindai katika Manispaa ya ameshauri vijana kutobagua kazi licha ya kuwa na elimu kubwa kwa sababu kazi yoyote ikipendwa, ikafanywa kwa ustadi na  nidhamu inaboresha maisha.

Elias ambaye mjini Singida ni maarufu kwa jina la Msukuma muuza Matunda, amebainisha kufanya kazi hiyo tangu Juni Mwaka 2013 baada ya kukopeshwa nanasi mbili na rafiki zake waliokuwa wakifanya bishara ya kutoa nanasi Geita, kuyauza Singida.

Ametaja marafiki hao kuwa ni Joseph na Mateso Chimvugu, ambao ni ndugu wazaliwa wa Mkoa wa Kigoma ambao pia walimsaidia kusafiri kutoka kwao Geita mpaka Singida na kumnunulia kindoo kidogo, alichokuwa akihifadhia nanasi alizokuwa akizikata katika vipande na kuviuza kwa wateja mitaani.

Baadaye alijiongeza kwa kuongeza matikiti maji na anasema miezi takriban sita baadaye alipata nafasi ya kujenga kibanda  pembezoni mwa stendi ya mabasi ya mkoa huo ambayo sasa inaitwa stendi ya zamani.

Mpaka sasa anaendelea kuuza aina tofauti za matunda kwenye eneo hilo, ambako amejenga kibanda kwa mbao kilichoezekwa bati na kwamba licha ya mtaji wake wa biashara kukua, anamudu kutunza familia yake yenye mke na watoto wanne.

Wakati mtoto wake wa kwanza kwa sasa ni askari polisi katika kikosi cha kutuliza ghasia (FFU), mtoto wa pili anasoma kidato cha tatu na wadogo zao wanasoma elimu ya msingi.

Anasema biashara hiyo imemuwezesha kujenga nyumba nyumbani kwao Geita, ambayo mama yake mzazi anaishi pamoja na wapangaji na pia mjini Singida amejenga nyumba anayoishi na familia yake na amenunua kiwanja maeneo  anayoishi.

Anabainisha siri ya mafanikio yake kuwa ni kutokata tamaa, bidii, kuipenda kazi yake na kuifanya kwa ustadi, lugha nzuri kwa wateja na kuwa na nidhamu katika matumizi ya kipato chake.

Hata hivyo anasema kama ilivyo kwa shughuli nyingine, biashara hiyo ina changamoto ambazo ili kukabiliana nazo inatakiwa kuwa makini wakati wa ununuzi na uuzaji wa bidhaa hizo.

Ili kuepuka hasara, anasema inatakiwa mtu kuwa mbunifu kwa kubuni mbinu tofauti zinazowezesha matunda yanunuliwe kwa haraka, kuepuka hasara endapo yataoza.

Yeye amekuwa akiuza tunda kama lilivyo lakini pia hukata vipande vya nanasi na tikiti maji na kuvifunga katika vifuko vya nailoni, ili yawe katika hali ya usafi na kuuza kila kipande Sh 500.

Aidha wateja wanaotaka kuchanganya aina tofauti za matunda na kuyala hapo hapo kwenye eneo lake la biashara, amekuwa akiwakatia kati aina ya matunda wanayotaka na kuwawekea kwenye sahani, huuza sahani moja Sh 1,000.

Parachichi

Kwa mujibu wa Elias, wafanyabiashara wa matunda mkoani Singida hununua maparachichi kwa misimu miwili; kuanzia Septemba mpaka Machi hununua maparachichi yanayotolewa nchini Burundi na kuanzia mwishoni mwa Machi mpaka Juni hununua maparachichi yanayotolewa Mkoa wa Kilimanjaro.

Anasema ni tunda linaloshika nafasi nzuri kwa kupendwa na kununuliwa ingawa katika miaka miwili iliyopita, limekabiliwa na changamoto ya kuvunwa kabla ya kukomaa, hali inayowasababishia hasara na kupoteza wateja.

Anasifia Parachichi zinazozalishwa Burundi, kwamba ni mbegu kubwa, ambapo parachichi moja huuzwa kati ya Sh 1,000 hadi 2,000 huku yale ya mbegu ndogo yakiuzwa kati ya Sh 400 hadi 700.

Maparachichi yanayonunuliwa kutoka Kilimanjaro, yanasifiwa na Elias kwamba yanaongoza kwa ubora, ingawa upatikanaji wake huwa wa muda mfupi yamekuwa yakiwapa faida nzuri kwa kuwa hupendwa zaidi na wateja na hayaharibiki hovyo.

Hivi karibuni, Mkurugenzi Msaidizi katika Idara ya Maendeleo ya Mazao ya Wizara ya Kilimo, Samson Poneja, alikaririwa na vyombo vya habari akiwa mkoani Njombe kulikodaiwa kuwapo maparachichi yaliyotupwa kwenye dampo la Halmashauri ya Njombe baada ya kubainika kukosa ubora.

Kwa mujibu wa Poneja, Wizara hiyo iliagiza timu ya wataalamu hao kufatilia kwa kufanya mahojiano na mdau aliyedaiwa kutupa Maparachichi hayo, wadau wengine na wakulima wa zao hilo ili kufahamu undani wa tukio hilo.

Anasema pia wizara ipo kwenye hatua za mwisho za kuandaa mwongozo, unaotoa dira kuhusu taratibu za msingi za kuzingatia, kuanzia uzalishaji mpaka uvunaji wa Parachichi kwa kuzingatia viwango ili kupata mavuno yenye ubora, yatakayohimili ushindani sokoni.

Akatoa wito kwa wakulima kutokubali ushawishi wa wachuuzi, kuuza maparachichi ambayo hayajakomaa kwa kuwa ndiyo chanzo kikuu cha kusababisha yakose ubora unaotakiwa.

Anasema Wizara hiyo imeshawishi wadau na kupata masoko ya zao hilo ndani na nje ya nchi, hivyo uwepo wa matukio ya aina hiyo unaweza kuathiri jitihada hizo jambo ambalo haliwezi kuvumilika.

Anasema taarifa kamili ya tukio hilo itatolewa kwa umma baada ya uchunguzi unaofanywa na wataalamu hao kukamilika, ikibainika ni tukio lenye lengo la kuathiri jitihada za wizara zilizofanikisha kupata masoko nje ya nchi, hatua za kisheria zitachukuliwa.

Naye Elias anasema hali ya baadhi ya wakulima kushawishiwa na wachuuzi na kuvuna maparachichi kabla hayajakomaa, ipo na inawasababishia hasara wafanyabiashara.

Anashauri elimu itolewe kwa wakulima wote nchini pamoja na wachuuzi ili kunusuru uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa.

Pia nawashauri vijana wasomi wajizuie kutawaliwa na kiburi cha usomi, watafiti na  kubaini kazi wanayoipenda hata kama ni tofauti na taaluma waliyosomea kwa sababu wakiifanya kwa ufanisi na wakawa na nidhamu katika matumizi ya kipato, watajikomboa kiuchumi.

Habari Zifananazo

Back to top button