Mkulima adakwa na mabomu, risasi 30 za AK47

POLISI mkoani Kigoma wamemtia mbaroni mkulima akiwa na mabomu mawili ya kurusha kwa mkono na risasi 30 za bunduki za kivita aina ya SAR/AKA 47 zikiwa kwenye magazine.

Kamanda wa polisi wa mkoa huo, Filemon Makungu alisema mwananchi huyo mkazi wa Kijiji cha Nyambemba Wilaya ya Buhigwe alikamatwa baada ya polisi kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema.

Kamanda Makungu aliwaeleza waandishi wa habari mjini Kigoma kuwa mkulima huyo ambaye sasa jina lake linahifadhiwa, alidaiwa kuchimbia silaha shambani na polisi walipofika kwenye eneo hilo walizikuta.

Advertisement

Alisema wamemkamata mmiliki wa shamba hilo ambaye jina lake limehifadhiwa wakati uchunguzi kuhusu tukio hilo ukiendelea.

Katika tukio lingine, Kamanda Makungu alisema wanawashikilia wakazi wawili wa Kibirizi Manispaa ya Kigoma Ujiji wakiwa na vipande 13 vya miundombinu ya reli.

Alisema watuhumiwa hao walikutwa na vipande vya vifaa vya reli na taruma la reli na hawakuwa na maelezo ya kujitosheleza kuhusu sababu ya kuwa na vifaa hivyo.

Pia alisema wamemkamata mkazi wa Mwanga Manispaa ya Kigoma Ujiji jina limehifadhiwa akiwa na vifaa vya kuvunjia nyumba na samani za ndani zinazoaminika kuwa ziliibwa kwenye nyumba za watu.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *