THOMAS Nkola maarufu kama mkulima na mfugaji amefungua maombi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya kuwashitaki baadhi ya mawaziri, wakuu wa taasisi za umma na kampuni binafsi.
Nkola ameomba kushitaki viongozi hao akidai wamehusika katika ubadhirifu wa fedha za umma katika ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Sh trilioni 8.4.
Amefungua mashauri matano ya maombi na tayari yamesajiliwa na kupangiwa mahakimu wa kuyasikiliza.
Wakili wa mkulima huyo, Penina Ernest amedai kuwa maombi hayo yanahusu ubadhirifu wa fedha za umma zilizotajwa katika ripoti ya CAG ya mwaka wa fedha 2021/2022.
Alidai kuwa mteja wake amefungua maombi hayo chini ya ibara ya 27 (1,2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977.
Alisema ibara hiyo inataka kila mtu alinde mali asili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mali ya mamlaka ya nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine.
Pia Penina alisema ibara hiyo inamtaka mwananchi atunze vizuri mali ya mamlaka ya nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu na kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa.
Alitaja baadhi ya watu aliowafungulia maombi hayo ni Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, Kamishna wa Usimamizi wa Madeni katika Wizara ya Fedha na Mipango, Japhet Justine, Mkurugenzi wa Mashitaka na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Salum Hamduni ambao anadai wameisababishia serikali hasara ya Sh trilioni 1.285.
Wengine ni Waziri wa Nishati, January Makamba, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Maharage Chande na mfanyabiashara, Habinder Seth ambao alidai wamesababisha hasara ya Sh bilioni 342.
Mwananchi huyo aliishukuru mahakama kwa kukubali kufungua mombi hayo.