MKULIMA wa kijiji cha Ihemi wilayani Iringa Asajile Mwanjala juzi amemkamata mnyama aina ya Kakakuona anayeaminika kufanya utabiri wa mambo mbalimbali yanayomzunguka binadamu na kuamua kumkabidhi kwa halmashauri ya wilaya hiyo, kitengo cha wanyamapori.
Hii ni mara ya pili kwa Mwanjala kumkamata akiwa katika shamba lake mnyama huyo ambaye ni nadra kuonekana, mara ya kwanza ikiwa ni mwezi mmoja tu uliopita na kuamua kumchukua na kumhifadhi nyumbani kwake baada ya kumtabiri mafanikio makubwa katika kilimo chake cha parachichi.
Hata hivyo Mwanjala alisema baada ya kumchukua na kumhifadhi nyumbani kwake, mnyama huyo alipotea katika mazingira ya kutatanisha.
Akizungumza wakati akimkabidhi mnyama huyo, Mwanjala alisema; “nilipomuona tena mnyama huyu ambaye sina hakika kama ndiye yule niliyemkamata kwa mara ya kwanza nilitoa taarifa Polisi kabla ya kumchukua na kwenda naye tena nyumbani.”
Alisema baada ya kutoa taarifa hiyo Polisi ndipo aliposhauriwa awasiliane na Idara ya Maliasili ya halmashauri hiyo na akafanya hivyo kabla ya kuwakabidhi.
Akizungumzia jinsi mnyama huyo anavyotabiri mambo mbalimbali, alisema alipomkamata kwa mara ya kwanza alimuwekea jani la parachichi, fedha na jembe lakini kakakuona huyo alishika jani la parachichi na hivyo kumfanya aamini atapata mafanikio kupitia zao la parachichi.
“Siwezi kusema kama nimeanza kuyaona mafanikio kwasababu ni mwezi mmoja tu umepita tangu anitabirie kupata mafanikio katika zao hili la Parachichi nalolima, lakini toka wakati huo naona mabadiriko fulani ya kutia moyo,” alisema.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ihemi, Stanley Castory alisema baada ya kupata taarifa ya uwepo wa Kakakuona huyo alifika eneo la tukio na kumsaidia Mwanjala kumtafuta Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ambaye alifika na timu ya wataalamu na kumchukua.
Kwa upande wake Afisa wa Wanyamapori wa halmashauri hiyo, Charles Mdendeme amesema Kakakuona ni mnyama asiye na madhara yoyote kwa binadamu hivyo akionekana katika maeneo yao watoe taarifa kama alivyofanya Mwanjala ili achukuliwe na kurejeshwa katika hifadhi yake.
“Kakakuona ni mnyama ambaye thamani yake inaweza kuwa kubwa kuliko Tembo na ndio maaana tunasisitiza wananchi wasiwadhuru kwa sababu ni nadra sana kuwaona na ukikutwa naye kinyume cha sheria kifungo chake ni miaka 30 na kuendelea,” alisema.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Bashir Muhoja alisema Kakakuona huyo atarejeshwa katika makazi yake halisi baada ya kukabidhiwa kwa Maafisa wa wanyamapori.
Aidha alisema kuwa baada ya Kakakuona huyo kumtabiria kijana huyo kupata mafanikio kupitia zao la Parachichi ofisi yake inawahimiza wananchi wengine kuwa na mwamko wa kulima zao hilo ili waweze kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla.