Mkulo aliliwa, kuzikwa leo Kilosa

DAR ES SALAAM; WAZIRI wa zamani wa Fedha na Mbunge wa zamani wa Kilosa, Mustafa Mkulo amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospital ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam.

Taarifa ilitolewa na familia yake jana imeeleza kuwa Mkulo alifariki dunia Mei, 3 mwaka huu na alisaliwa swala jana katika Msikiti wa Maamur, Upanga Dar es Salaam.

Ilieleza kuwa safari ya kwenda Kilosa ilianza jana baada ya swala ya adhuhuri na maziko yanafanyika leo nyumbani kwake Kilosa mkoani Morogoro.

Advertisement

Viongozi waliojitokeza kumuaga Mkulo nyumbani kwake Mikocheni, Dar es Salaam ni; Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri wa Elimu wa zamani na Skauti Mkuu mstaafu, Mwantumu Mahiza na mwanasiasa Mohamed Thabit Kombo.

Isome pia:https://habarileo.co.tz/mustafa-mkulo-afariki-dunia/

Wengine ni waziri wa zamani Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, aliyewahi kuwa mbunge wa viti maalumu, Zainab Vullu, mbunge wa viti maalumu, Najma Giga na Mshauri wa Rais, Sophia Mjema.

Mkulo alizaliwa Septemba 26, 1946. Alikuwa mbunge wa Kilosa kwa miaka 10 hadi mwaka 2015 kabla ya kuamua kutogombea.

Aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Waziri wa Fedha mwaka 2007 hadi 2012. Mei 2012, Mkulo alikuwa miongoni mwa mawaziri sita walioachwa katika uteuzi wa Baraza la Mawaziri katika serikali ya awamu ya nne.

Aliwahi kufanya kazi ofisi tofauti ndani ya serikali ikiwamo Shirika la Taifa na Maendeleo(NDC), Ofisi ya Msajili wa Hazina na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) akiwa ni mkurugenzi.