DODOMA: WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo amesema, serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) haitetei wezi na ina historia katika kuwachukulia hatua wezi ambao wanabainika hata kama walikuwa ni viongozi wa serikali.
Mkumbo ameyasema hayo leo Novemba 4, 2023 bungeni mjini Dodoma na kudai kuwa hakuna Waziri anayeikataa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
“Kuna hatua kadhaa zimechukuliwa ikiwemo viongozi waliobainika kwa wizi kufikishwa mahakamani na kufungwa na kuongeza kuwa utekelezaji wa jambo hilo halijaanza leo” amesema na kuongeza
“Tunaposimama kujibu hoja isionekane tunatetea majambazi, serikali ya CCM ilishawahi kuwafunga mawaziri, suala la kuwapeleka mahakamani wezi na majambazi kwa CCM halijaanza leo. Wapo mawaziri na makatibu wakuu walishafikishwa mahakamani, muhimu ni kwamba lazima sheria zifuatwe” amesisitiza.
Aidha, Prof. Mkumbo ameng’aka kuwa wanaodai nchi inakufa itakufaje wakati miradi mikubwa ya maendeleo inaendelea kujengwa
“Kuna Mbunge anasema eti nchi inakufa, katika political science (Sayansi ya Siasa) ni failed state, unasemaje nchi inakufa wakati inajenga reli yenye urefu wa kilometa 2,600 kutoka Dar es Salaam hadi Karema? Unasemaje nchi inakufa wakati imetoa Rais wa IPU (Umoja wa Mabunge Duniani).” Amesema kwa kuhoji na kuongeza
“Nchi ambayo dunia nzima inaiamini na kukubali Spika wake awe ndio Rais wa IPU unasemaje inakufa?”
“Kuna mtu anasema namnukuu “na leo nasisitiza kuwa tumepigwa zaidi ya Sh trilioni 280”, mimi kama Waziri wa Mipango ninayefahamu kuwa pato lote la nchi hii ni Sh trilioni 141.
“Ukitoka Kagera hadi visiwani Pemba ukikusanya fedha zote ni sh trilioni 141 halafu kuna mtu anasema zimepigwa trilioni 280, how (kivipi)?. Logic (mantiki) inakataa, ni hoja ambayo haina mantiki.
Prof Mkumbo alikuwa akijibu kauli ya Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina akichangia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) akidai kuwa usalama wa kifedha ‘Financial Intellegence Unit’ (FIU) inaonyesha zaidi ya sh trilioni 280 zimetakatishwa.
Akichangia Mpina amesema utakatishaji wa fedha haramu, ufadhili wa ugaidi, na ufadhili wa silaha za maangamizi, taarifa ya FIU (financial intelligence unit) inaonyesha fedha taslimu na zile zilizopitia kwenye miamala ya simu zaidi ya Sh trillion 280 hadi Aprili 25 mwaka huu ni haramu.
Alihoji “hivi utawezaje kukusanya fedha katika nchi ambayo ina fedha haramu zaidi ya Sh trilioni 280?
“Maana yake kuna ukwepaji wa kodi uliopitiliza, kuna ‘financial cash flow’ ‘utoroshaji wa fedha nje ya nchi nyingi’ uliyopitiliza, kuna ‘transfer financial un illegal’ zilizopitiliza utakusanyaje kodi katika mazingira kama hayo? Alihoji Mpina.