Mkurabita yaanza kurasimisha biashara ya bodaboda

MRATIBU wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), Dk Seraphia Mgembe amesema mwaka huu wamerasimisha biashara ya bodaboda ili kuliwezesha kundi hilo kutambulika rasmi kama zilivyo tasnia nyingine.

Aidha, urasimishaji huo utaondoa migogoro ya mikataba kati yao na wamiliki wa vyombo hivyo.

Dk Mgembe amesema hayo jijini hapa wakati wa kutoa mada kwenye semina kwa wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI).

“Mkurabita umekuwa ukitekeleza majukumu yake ya urasimishaji wa ardhi vijijini na kujenga masijala, urasimishaji ardhi mijini, kujenga vituo vya urasimishaji na urasimishaji wa biashara na kwa mwaka huu tumefikia kurasimisha biashara ya bodaboda,” alisema.

Dk Mgembe alisema katika kurasimisha biashara ya bodaboda, halmashauri sita zimefikiwa ikiwemo Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Halmashauri zingine ni Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Halmashauri ya Rungwe na Halmashauri ya Tarime Mji.

Dk Mgembe alisema kupitia mpango huo wa kurasimisha bodaboda, waendesha bodaboda 6,365 wamepata mafunzo huku vituo vya bodaboda vipatavyo 264 vikisajiliwa.

Alisema pia leseni 3,014 huku serikali ikipata mapato ya Sh milioni 30.14 kutokana na utolewaji wa leseni hizo.

Wadau wa urasimishaji biashara ya bodaboda ni halmashauri, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu (LATRA), Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), taasisi za fedha na umoja wa waendesha bodaboda.

Akizungumzia matokeo kwa wananchi yaliyotokana na urasimishaji wa biashara ya bodaboda, alisema waendesha bodaboda wamekopa zaidi ya Sh milioni 880.

Serikali inatekeleza Mpango wa Mkurabita kwa lengo la kuwezesha wananchi kurasimisha rasilimali na biashara zao, kuwezesha upatikanaji wa mitaji na kuwawezesha Watanzania wengi kushiriki katika fursa za kiuchumi.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button