Mkurugenzi apewe siku 6 kituo cha afya Mikese kutoa huduma

OFISI ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( TAMISEMI) imemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kuwa ifikapo Februari 13, 2023 Kituo Afya cha Mikese kiwe kinafanya kazi ya kuwahudumia wananchi kutokana na kukamilika kwa asilimia 100.

Naibu Katibu Mkuu Tamisemi anayeshughulikia sekta ya afya, Grace Magembe alitoa agizo hilo jana kwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo , Ndelisho Moshi pamoja kwa ganga mfawidhi wa hospitali ya halmashauri hiyo.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo alilolitoa kwenye ziara yake hivi karibu katika halmashauri hiyo.

Naibu Katibu Mkuu Tamisemi sekta ya afya alifanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Afya hicho na kujionea hali ya utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wa tarafa ya Mikese.

Magembe alisema ujenzi wa kituo hicho umekamilika kwa asilimia 100 na suala lililobakia ni utoaji wa huduma kwa wananchi na kuagiza kushughulikiwa vifaa tiba na dawa ili wananchi wapate huduma mara moja.

Alisema serikali ilitoa fedha sh millioni 400 za ujenzi wa majengo matano ilikiwemo la huduma ya mama na mtoto, maabara, wodi ya wazazi na jengo la dharura na ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100.

“Nataka kuanzia Jumatatu Februari 13, mwaka huu (2023) huduma ya Afya kwa wananchi wa Tarafa ya Mikese ianzekutolewa katika Kituo cha Afya Mikese kutokana na kukamilika kwa miundombinu yote muhimu” alisema Magembe

Naibu Katibu Mkuu huyo akiwa kwenye Zahanati ya Kijiji cha Fulwe aliwahimiza wananchi kujiunga na bima ya afya iliyoboreshwa ili waweze kupunguza gharama za matibabu ambazo wanakutana nazo.

Naye Diwani wa Kata ya Mikese , Saidi Kimbeho ameeleza halmashauri inakabiliwa na changamoto ya gari la kubebea wagonjwa kwani kwa sasa lipo moja kwa halmashauri zima na inaleta shida pele wagonjwa wengi wanaopata rufaa kwenda hospitali ya Rufaa kwa matibabu zaidi.

Akiwa kwenye ziara ya mkoa wa Morogoro ambayo ilifikisha katika halmashauri hiyo, Katibu mkuu wa CCM,Chongolo alikasirishwa na kutelekezwa kwa Kituo cha Afya hicho kilichokamilika zaidi ya miaka mitatu sasa lakini hakitumiki kutoa huduma kwa wananchi.

Katibu mkuu wa CCM alimpa siku 14, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,(TAMISEMI) Angellah Kairuki, kufika kituoni hapo kujionea hali halisi.

Chongolo alikerwa na hali hiyo na kusema serikali imepeleka fedha ili wananchi wake wapate huduma lakini baadhi ya watendaji hawatimizi wajibu wao hali inayofanya pia baadhi ya watu waanze kumsimanga Rais Dk Samia Suluhu Hassan.

“Watu wetu hapa wanakaa kienyeji hawatimizi wajibu wao,nitawasiliana na Waziri wa Tamisemi na ndani ya siku 14,aje hapa ajionee,vifaa vipo vimekaa tu wakati huduma zinatakiwa zitolewe,”alisema Chongolo.

Kwa mujibu wa taarifa fupi ya ujenzi wa kituo hicho, iliyotolewa na Kaimu Mtendaji wa Kata ya Mikese, Piencia Mushi kwa Katibu mkuu wa CCM, kuwa ujenzi huo ulianza mwaka 2019 baada ya kubomolewa kwa Zanahati ya Kijiji ili kupisha ujenzi wa Reli za Kisasa ya (SGR).

Mushi alisema ujenzi ulianza kufanywa na Kampuni ya Yapi Merkez iliyotakiwa kulipa fidia ya zahanati iliyobomolewa kupisha ujenzi wa reli hiyo na gharama za jengo ulikuwa Sh milioni 105 na vifaa tiba gharama zilikuwa Sh milioni 200.

Alisema awamu ya pili ujenzi wa majengo yakiwemo ya chumba cha upasuaji, nyumba ya mtumishi, maabara, chumba cha kuhifadhi maiti na jengo la mama na mtoto umegharimu Sh milioni 400 na halmashauri ikaongezea sh milioni 60.5

Kwa mujibu wa Kaimu Mtendaji kata huyo kuwa pamoja na hayo yote, bado kituo hicho hakitumiki na huduma zinazotolewa ni zile za kiwango cha zanahati.

Habari Zifananazo

Back to top button