Mkurugenzi Iringa akingiwa kifua

MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Stephen Mhapa amemkingia kifua mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Bashir Muhoja anayelalamikiwa kutokuwa na mahusiano mazuri ya kiutendaji na baadhi ya madiwani na Chama cha Mapinduzi (CCM), wilaya ya Iringa.

Hatua hiyo imekuja miezi miwili baada ya Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Iringa kutangaza kutokuwa na imani naye katika kikao chake kilichofanyika Januari 25, mwaka huu.

                       Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Stephen Mhapa akifafanua jambo

Katika kikao hicho, Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Constantino Kiwele alisema mbali na kulalamikiwa na madiwani kadhaa wa halmashauri hiyo, Mkurugenzi huyo hana mahusiano mazuri na chama jambo linaloathiri ufuatiliaji kikamilifu wa utekelezaji wa Ilani.

Alisema yeye binafsi kama mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo hakumbuki ni lini mkurugenzi huyo alipokea simu yake au kumpigia katika kile kinachohusu; “Mafanikio na changamoto zinazohusu utekelezaji wa Ilani.”

                         Mkurugenzi wa Halmashauri Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Bashir Muhoja.

Kiwele alimshtaki mkurugenzi huyo kwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Salim Asas akimuomba kwa kupitia vikao vyao vya juu wachukue hatua zitakazosaidia kunusuru yanayoendelea.

Katika kile kinachoelezwa kwamba sio sahihi kwake kujibu hadharani malalamiko ya chama anachokisaidia kutekeleza Ilani yake, mkurugenzi huyo amekuwa akijiweka kando na wito wa vyombo vya habari ambavyo mara kwa mara vimekuwa vikihitaji ufafanuzi wake.

Mmoja wa madiwani wanaolalamikia utendaji wa mkurugenzi huyo, Diwani wa Kata ya Ilolompya Fundi Mihayo amenukuliwa mara kadhaa akisema wanapita katika kipindi kigumu cha ufanyaji kazi na mtendaji huyo na akaomba taarifa ya CCM dhidi yake ifanyiwe kazi.

                                     Mwenyekiti wa CCM  Wilaya hiyo, Constantino Kiwele

Baada ya Asas kuyachukua malalamiko hayo na kuahidi kuyafikisha katika kikao cha Kamati ya Siasa ya Mkoa ambayo mmoja wa wajumbe wake nu Mkuu wa Mkoa, jana Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa amesifia utendaji wa mkurugenzi huyo akisema ni wa kupigiwa upatu.

“Nimshukuru sana Mkurugenzi wa Halmashauri, ni mkurugenzi mzuri sana, bora sana na mwenye uwezo mkubwa sana,” Mhapa alisema katika kikao cha wadau wa elimu wa halmashauri hiyo huku akipigiwa makofi na baadhi ya madiwani.

Akiendelea kumwaga sifa za uwezo wa mkurugenzi huyo alisema; “Mimi ndio msimamizi wa halmashauri hii, nimekaa na wakurugenzi wengi, huyu jamaa ni wa  tofauti sana, anaweza kutoka nyumbani kwake hata saa 11.00 Usiku kufuatilia mambo ya maendeleo.”

Akitolea mfano wa ubunifu wake, Mhapa alisema katika kuiboresha sekta ya elimu mkurugenzi huyo ndiye aliyetoa wazo la kupaua kwa vyuma badala ya mbao madarasa yaliyojengwa kwa fedha zilizotolewa na serikali ya Dk Samia Suluhu Hassan kwa kupitia mpango wa kukabiliana na Covid 19.

“Ubunifu wako Mkurugenzi utaifanya halmashauri yetu isahahu kukarabati madarasa hayo kwasababu hakuna mchwa anayeweza kushambulia chuma, kwahiyo tuna madarasa yatakayodumu kwa muda mrefu,” alisema.

Mhapa aliendelea kumsifia mkurugenzi huyo akiwataka wataalamu wasiogope kuwashauri wanasiasa mambo yanayoweza kuwa na faida ya kizazi kilichopo na kijacho kwa maendeleo ya Taifa.

“Tunakupongeza mkurugenzi na watumishi wako wote, peleka salamu hizi kwa watumishi wako. Changamoto ni jambo la kawaida na hushughulikiwa-Mungu akubariki sana na akupe maisha mazuri kwasababu unafanya kazi nzuri,” alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button