MSHITAKIWA Peter Gasaya (32), ambaye ni Mkurugezi Mtendaji wa Kampuni ya Jatu Public limited anayekabiliwa na shitaka la kujipatia fedha tasilimu Sh 5,139,865,733.00 kwa njia ya udanganyifu, amefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa ajili ya kupewa masharti ya dhamana.
Wakili wa serikali Tumaini Maingu alieleza mahakama leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Mery Mrio anayeisikiliza kesi hiyo, ambapo alidai kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya mshitakiwa kupewa masharti ya dhamana, baada ya siku nne kupita tangu alipofikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza akikabiliwa na shitaka hilo.
Baada ya kusikiliza maombi hayo Hakimu Mrio alitoa masharii matatu dhidi ya mshitakiwa huyo, ambapo alitakiwa kuwasilisha fedha taslimu Sh 2,600,000,000 au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.
Pia alitakiwa awe na wadhamini wawili wanaotambuliwa kisheria ambao watakuwa na barua kutoka serikali za mtaa, ikiwa imeambatanishwa na kitambulisho cha Taifa au cha mpiga na wawe wakazi wa Dar es Salaam.
” Wadhamini hawa wanatakiwa kusaini nusu ya mali iliyotajwa kwenye hati ya mashtaka au kuwasilisha hati ya mali yenye thamani ya Sh 2,600,000,000 na hati hiyo itabidi ihakikiwe kwanza kabla ya kuletwa mahakamani hapa,” alisema Mrio.
Hata hivyo mshtakiwa ameshindwa kutimiza masharti hayo na kurudishwa rumande hadi Januari 11, 2023 kesi hiyo itakaporudi kwa ajili ya kutajwa.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka inadaiwa kuwa katika terehe isiyofahamika kati ya Januari mosi na Desemba 31, mwaka 2021 ndani ya mkoa wa Dar es salaam Mshitakiwa akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Jatu Public Limited, alijipatia Sh 5,139,865,733.00 kutoka Saccos ya Jatu akijinasibu kukizalisha kiasi hicho cha fedha kwa kuwekeza fedha katika kilimo cha faida wakati akijua si kweli.
Mshitakiwa alipandishwa kizimbani Desemba 29, mwaka 2022 akikabiliwa na shitaka la kujipatia fedha tasilimu shilingi 5,139,865,733.00 kwa njia ya udanganyifu.