Mkurugenzi Mafinga ataka uwazi mapato na matumizi
MKURUGENZI mpya wa Halmashauri ya Mji Mafinga, Ayubu Kambi ameanza kutaja vipaumbele vyake vitakavyomuwezesha kusimamia vyema utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ili wananchi wa mji huo wapate maendeleo yaliyokusudiwa.
Katika kikao chake alichofanya kwa nyakati tofauti na watumishi wa kata ya Bumilayinga na Isalavanu toka ateuliwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo hivikaribuni, kambi amesema uwazi wa mapato na matumizi ya halmashauri ni moja ya vipaumbele vyake katika kufikia malengo ya serikali katika mji huo.
“Hakikisheni mnaweka wazi na kuwasomea wananchi kwenye mikutano ya kata na vijiji fedha zote mnazopokea kwa ajili miradi ya maendeleo na kubandika kwenye mbao za matangazo kwani ni haki ya wananchi kujua mapato na matumizi na kufahamu miradi gani katika maeneo yao serikali inatekeleza,” alisema.
Amewataka watendaji wa kata na vijiji katika halmashauri yake kufanya kazi na kuwajibika kikamilifu ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa hizo za fedha zinazotolewa na serikali, wafadhili na michango na nguvu za wananchi.
Alisema hatua hiyo itaongeza uwajibikaji, uwazi na kuleta imani kwa wananchi kushiriki katika michango na utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Akipokea changamoto za watumishi, Kambi alisema katika utumishi kuna haki na wajibu, na akawataka watumishi hao kuzingatia mambo hayo mawili ili kuweka sawa mizania ya wanachohitaji na wanachofanya.
“Nimepokea changamoto zenu na nitazifanyia kazi na ndio mana nimekuja na wataalamu wangu ili zile zinazoweza kushughulikiwa tuzimalize na zile zinazohitaji ufuatiliaji tuzichukue,” alisema katika vikao hivyo vilivyohudhuriwa na wataalamu wa idara ya Utawala, Elimu Msingi na Sekondari.
Akizungumzia namna ya kushughulikia malalamiko ya wananchi wa ngazi ya kata kwa kutumia lugha nzuri mkurugenzi huyo ameagiza wataalamu wa halmashauri hiyo kufanya ziara na kutoa ufafanuzi kuhusu masuala ya haki za watumishi na sera mbalimbali ili kuwajengea uelewa watumishi ngazi ya kata.