Mkurugenzi PURA azuru shule ya msingi Likong’o kujionea utekelezaji wa CSR

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Charles Sangweni ametembelea Shule ya Msingi ya Likong’o iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Lindi kujionea hali yake pamoja na utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa madarasa mapya kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) na wabia wengine.

Wadau wengine wanaoshiriki katika uboreshaji wa mazingira ya kujifunzia katika shule hiyo ni kampuni za Equinor na Shell.

Sangweni alitembelea shule hiyo Jumatano (19 Julai, 2023) akiwa katika ziara ya kikazi kuelekea Halmashauri ya Mtwara Vijijini ambako alikutana na diwani wa Kata ya Likong’o, wajumbe wa kamati mbalimbali za Serikali za Mtaa pamoja na baadhi ya viongozi wa shule hiyo akiwemo mkuu wa shule hiyo, Shafii Said.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa PURA alisema kuwa mamlaka hiyo inafuatilia kwa karibu suala la utekelezaji wa CSR kwa kampuni ya mafuta, ikiwemo ujenzi wa madarasa mapya katika shule hiyo, moja ya mambo yaliyoainishwa katika mpango wa uwajibikaji kwa jamii wa TPDC na wabia wake katika mwaka 2023.

“Ujenzi wa madarasa mapya katika shule hii ni jambo ambalo limechukua muda mrefu tangu kuanza kufanyiwa kazi. Ni matamanio yetu kuona utekelezaji unafanyika mwaka huu na ndio maana tumeamua kulifuatilia kwa karibu,” aliongeza Sangweni.

Akizungumza katika kikao kifupi kilichofanyika wakati wa ziara hiyo, Diwani wa Kata ya Mbanja, Thabiti Ngwame alisema kuwa suala la ujenzi wa madarasa katika shule hiyo linapaswa kufanyiwa kazi na kufikiwa tamati kwa kuwa ni suala ambalo limekuwa na mlolongo usioisha.

Naye Mkuu wa shule hiyo alisisitiza ujenzi wa madarasa hayo unapaswa kuanza mapema kwani yaliyopo yana hali mbaya.

Likong’o ni eneo lililopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi ambako ndipo mradi wa kusindika gesi asilia (LNG) utatekelezwa.

Mradi huo unaokadiriwa kuwa na uwekezaji wa takriban Shilingi trilioni 97 unatarajiwa kuleta fursa nyingi kwa Watanzania zikiwemo ajira na utoaji wa huduma mbalimbali wakati wa ujenzi na uendeshaji wa mradi.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button