Mkutano mkuu wa CPC kuzingatia utulivu na mwendelezo wa sera

Tarehe 16 Oktoba China itakuwa mkutano mkuu wa chama cha kikomunisti cha China unaofanyika mara moja kila baada ya miaka mitano, ambao kazi yake kubwa ni kupanga mwelekeo wa chama katika kipindi cha miaka mitano.

Mkutano huu unafanyika katika wakati hali ya ndani ya China na hali ya kimataifa, ina changamoto mbalimbali kiuchumi na kiusalama, kwa hiyo kitakachojadiliwa na kuamuliwa kwenye mkutano huo, sio kama tu kitakuwa na umuhimu mkubwa kwa China yenyewe, bali pia kitakuwa na umuhimu mkubwa kwa dunia.

Kwa wachina, kinachofuatiliwa zaidi ni kama mafanikio ya kiuchumi, neema na usalama waliokuwa nao katika kipindi cha miaka mitano hadi kumi iliyopita vitalindwa au kuimarishwa na maamuzi yatakayofikiwa kwenye mkutano huo.

Kwa watu wengine wa nje ya China, kinachofuatiliwa zaidi ni kama maamuzi ya mkutano huo yatakuwa ya kuijenga China kuwa nchi yenye mchango katika kukabiliana na changamoto za dunia, na kuendelea kuifanya China kuwa moja ya nguzo muhimu za kufufuka kwa uchumi wa dunia na injini ya maendeleo ya dunia.

Kutokana na nafasi ya China katika uchumi wa dunia, mkutano huo umekuwa na ufuatiliaji mkubwa kuhusu mkutano huo karibu katika kila nchi.

Hili bila shaka ni shinikizo kwa wajumbe watakaohudhuria mkutano huo, kwa kuwa maamuzi watakayofanya hayatakuwa kwa ajili yao peke yao, chama chao au nchi yao, bali yatagusa dunia nzima.

Kwa wanaofuatilia kwa karibu siasa za China na maendeleo yake ya kiuchumi, bila shaka watakuwa wanajua ni nini kimefanyika nchini China katika miaka kumi iliyopita, na mchango binafsi wa Xi Jinping amekuwa na mchango gani katika hayo yaliyofanyika.

Kwa wasioelewa mchango binafsi uliotolewa na Rais Xi kwenye mafanikio yaliyopatikana nchini China miaka 10 iliyopita, wanatakiwa kuangalia hali ya uchafuzi wa hewa katika miji ya China kwa sasa na miaka 10 iliyopita, hali ya ufisadi miaka 10 iliyopita na sasa, hali ya umasikini hasa vijijini ilivyokuwa miaka 10 iliyopita, na hata changamoto za usalama katika baadhi ya mikoa ya magharibi mwa China ilivyokuwa.

Vile vile tunatakiwa kukumbuka kuwa mafanikio ya China katika kipindi hicho, sio kama tu yamefanya watu wa China waishi katika hali ya neema kiasi, bali pia yamefanya watu wa nchi nyingine wanufaike na maendeleo ya China.

Kwa nchi zetu za Afrika, China imekuwa ni mbadala mzuri wa vyanzo wa uwekezaji wa moja kwa moja, imekuwa ni soko kubwa na linalopanuka kwa mazao yetu ya kilimo, imekuwa mshirika mkubwa wa biashara na mdau mkubwa kwenye kuendeleza kandarasi mbalimbali za ujenzi zinazobadilisha sura ya miji yetu.

Kwa hiyo tupende tusipende mwelekeo wa China katika miaka mitano au kumi ijayo, unahusiana moja kwa moja na maendeleo ya nchi zetu.

Baadhi ya wachambuzi wa siasa kutoka kwenye nchi zinazofuata demokrasia ya kimagharibi, wamekuwa na maoni tofauti kuhusu kinachotarajiwa kufanyika kwenye mkutano huo.

Tukubaliane na ukweli kwamba, siasa za China ni tofauti sana na siasa za nchi za magharibi huwezi kuona mwanasiasa akizunguka kila mji na kupanda kwenye majukwaa ya kisiasa kuanza kuomba kura, lakini hii haina maana watu wanajiweka madarakani wenyewe, na kuamua kuwa madarakani kama wanavyopenda. Wachina wanafanya maamuzi kulingana na mahitaji ya nchi yao na wakati.

Mwezi Mei mwaka 2017 wakati wa mjadala mkali kuhusu vitendo vya kujilinda kibiashara kati ya nchi kubwa za magharibi, Rais Xi Jinping alijitokeza na kusema “hakuna nchi duniani inayoweza kutatua changamoto zote au kukabiliana na matatizo yote ya dunia peke yake” bila kujali nchi hiyo ni kubwa kiasi gani na ina nguvu kiuchumi kiasi gani, ndio maana Rais Xi Jinping alisema ni kwa kujenga uchumi ulio wazi, kuwa biashara huria na shirikishi, na kupinga vitendo vya kujilinda kibiashara, ndipo dunia inaweza kukabiliana kwa ufanisi na changamoto za uchumi, na hata changamoto nyingine.

Hicho ndio ambacho serikali ya China imekuwa ikikifanya katika miaka mitano iliyopita, na ndio kinachotarajiwa kuendelea kufanya bila kujali CPC inampa nani ridhaa kukiongoza chama.

Mbali na changamoto za kiuchumi zilizoendelea kuwepo tangu kuibuka kwa vitendo vya kujilinda kibiashara, na zilizofuata baada ya kutokea kwa janga la COVID-19, changamoto nyingine zimetokea na kufanya dunia iwe katika wakati mgumu zaidi.

Vita ya Ukraine imeleta hali ya sintofahamu kiusalama na kiuchumi sio tu kwa nchi za Ulaya bali katika sehemu nyingine duniani, na sasa watu wanazungumzia msukosuko wa kupanda kwa gharama karibu duniani, tunaona pia athari za mabadiliko ya tabia nchi zimeanza kuwa wazi kwa maisha ya watu na kuathiri uchumi,.

Hakuna nchi katika pembe yoyote ya dunia iliyo immune dhidi ya changamoto hizi, China pia ni mhanga wa matokeo ya changamoto hizi.

Wakati CPC inajiandaa kwa ajili ya mkutano huo, wachina wanajua kuwa wao ndio watakaoamua kama wanataka kuendelea na mwelekeo wa mafanikio waliyopata katika miaka kumi iliyopita, au kama wanataka kufuata njia nyingine.

Mpunji ni Mwandishi wa habari aliyeko Beijing, China

Habari Zifananazo

Back to top button