‘Mlalamikaji hahusiki kumsafirisha mtuhumiwa’
SERIKALI imebainisha kuwa kitendo cha mlalamikaji kulazimishwa kugharamia usafirishaji wa mtuhumiwa au mahabusu kwenda na kurudi rumande ni kukiuka sheria na kanuni zilizopo.
Haya yameelezwa bungeni jana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage (CCM). Katika swali lake, Mwijage alihoji ni kwa nini katika Tarafa ya Kamachumu mlalamikaji hulazimishwa kumgharamia mahabusu kwa kumsafirisha kwenda na kurudi rumande.
Akijibu swali hilo, Sagini alisema kitendo hicho ni kinyume na sheria na kanuni zilizopo na kinapaswa kuachwa mara moja. Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Polisi, Sura ya 322 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002 na Kanuni 353 na 354 ya Kanuni ya Jeshi la Polisi zinazosimamia watuhumiwa au mahabusu walioko kwenye vituo vya polisi, zinaeleza wazi utaratibu wa kuwasafirisha watuhumiwa au mahabusu kwenda mahakamani hutekelezwa na Jeshi la Polisi.
Sagini alisema jukumu la kuwasafirisha watuhumiwa au mahabusu kutoka rumande gerezani kwenda mahakamani ni jukumu la Jeshi la Magereza kwa mujibu wa Kifungu cha 75 cha Sheria ya Magereza Sura ya 58 ya mwaka 1967 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.
“Wizara imefanya mawasiliano na Wakuu wa Vyombo vyetu yaani Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na Mkuu wa Jeshi la Magereza (CGP) ili wawaelekeze wasaidizi wao ngazi za mikoa na wilaya kuzingatia sheria.”