Mlinzi gesti auawa na watu wasiojulikana

MLINZI wa nyumba ya kulala wageni katika Kijiji cha Buseresere, Kata ya Buseresere Halmashauri ya Wilaya ya Chato mkoani Geita amekutwa ameuawa na watu wasiojulikana kwa kupigwa na kitu kizito.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Buseresere, Deus Musiba alisema tukio hilo ni la alfajiri Februari 11, 2023 katika nyumba ya kulala wageni ya Kings.

Alisema taarifa za tukio hilo zilipokelewa saa 1:00 asubuhi ambapo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi walifanya uchunguzi wa awali na kubaini mlinzi huyo alikuwa na jeraha shingoni.

Advertisement

“Yule mtu aliyeuawa, amepigwa na kitu kizito sehemu ya taya karibu na sikio, ametokwa na damu nyingi kiasi cha watu kuanza kuhisi amechinjwa.”

“Polisi walikuja na kufanya uchunguzi na kujiridhisha hakuwa amechinjwa, isipokuwa alikuwa amepigwa na kitu kizito na kutokwa na damu nyingi,” alieleza mwenyekiti huyo.

Alisema uchunguzi pia ulibaini watuhumiwa walivunja kufuli kwenye geti la nyumba hiyo ya kulala wageni, kisha kuingia ndani na kufanya mauaji hayo.

“Hawakuchukua kitu chochote, hawakuharibu kitu chochote, wamefanya hivyo na wakaondoka, mpaka sasa tunafanya uchunguzi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama,” alisema.

Mhudumu wa nyumba hiyo ya kulala wageni, Dativa Mathias alisema aliamka majira ya saa 11:00 alfajiri na kushangaa kutomkuta mlinzi kwenye chumba cha mlinzi na ndipo alimuona amefariki dunia getini.

Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Katoro, Dk Zakayo Sungura alithibitisha kifo cha mlinzi huyo na kueleza kuwa anatambulika kwa jina moja la Mashaka.

“Mwili ulikuwa na majeraha katika sehemu ya kichwani na shingoni, kifo chake kimetokana na kuvuja damu nyingi na majeraha yanaonekana yametokana na kupigwa na kitu kizito,” alisema.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita ili kupata kiini cha tukio hilo, hakupatikana.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *