MLINZI Bakari Kasarani (46) wa kampuni binafsi ya ulinzi aliyekuwa akilinda msikiti wa Shree Hindu Mandal Temple uliopo mjini Kahama mkoani Shinyanga, ameuawa kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana.
Ilidaiwa kuwa mlinzi huyo alivamiwa Machi 30, mwaka huu usiku akiwa eneo hilo na kufanyika uharibifu wa vitu vya thamani mbalimbali vilivyokuwa ndani ya msikiti huo.
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Shinyanga ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme ilifika kwenye eneo hilo juzi asubuhi baada ya kupata taarifa ya tukio hilo.
Mndeme alilaani tukio la uvamizi wa msikiti na mauaji ya kikatili yaliyofanyika ambapo alielezwa mlinzi huyo ana kipindi cha miaka zaidi ya 10 akifanya ulinzi kwa uaminifu kwenye msikiti huo.
“Serikali imesikitishwa na tukio hilo ambapo watu waliofanya kitendo hicho kiovu watafutwe mara moja popote walipo,” alisema Mndeme.
Alisema serikali itagharamia uharibifu uliofanywa ndani ya msikiti huo.
Msimamizi wa msikiti huo, Niraj Kakad alieleza kukuta mlinzi akiwa nyuma ya msikiti huo tayari ameuawa na vitu ambavyo bado thamani yake haijajulikana kuvunjwa ikiwemo sanamu inayoabudiwa.
“Tuliamka asubuhi tukakuta mlinzi ameuawa na vitu vimesambazwa ndiyo tukachukua hatua ya kwenda kutoa taarifa polisi,” alisema Kakad.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa aliiomba serikali kufanya uchuguzi wa kina wa tukio hilo ili waliohusika wafikishwe kwenye mkono wa sheria.