MWENYEKITI wa Halmashauri ya wilaya ya Geita, Charles Kazungu amewaomba maofisa mifugo kuchunguza haraka ugonjwa wa midomo na miguu ya ng’ombe ulioripotiwa katika baadhi ya maeneo kwenye halmashauri hiyo.
Kazungu ameeleza hayo wakati akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani cha mwisho wa robo ya kwanza ya mwaka 2022/23 na kueleza kuwa ugonjwa huo ni tishio jipya kwa wafugaji wilayani Geita.
Amesema ugonjwa huo usiojulikana umeonekana kusambaa kwa kasi na huenda ukaathiri wafugaji kwa kiasi kikubwa hivyo wataalamu wa mifugo wachukue juhudi kunusuru afya ya ng’ombe na walaji.
“Mifugo hii ndio inawasadia kulima wafugaji wetu, sasa itakapoteketea tutakuwa moja tumepungukiwa chakula, pili tutakuwa tumepungukiwa mboga pamoja na vitu vingine.” Amesema
Aidha, amewataka wafugaji kuhakikisha wanachanja mifugo yao kuwakinga na magonjwa na kuachana na tabia ya kupatia chanjo mifugo michache na kuacha mingine nyumbani.
“Tujitahidi ng’ombe zako zilizoathirika ziwe za kwako, tusichanganye na ng’ombe za kaya nyingine ama zizi lingine. Niombe tu wataalamu muingie kazini kuanzia leo.” Ameelekeza
Kaimu Ofisa Kilimo na Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Israel Tarima amekiri kuwepo kwa ugonjwa unaoathiri midomo na miguu ya ng’ombe na kwamba tayari wametoa taarifa kwa maofisa chanjo ili kubaini aina ya kirusi hicho.
“Ni kweli mlipuko wa ugonjwa kwenye kata tatu tumeshaupata ofisini kwetu, na tunaendelea kuwasiliana na wataalamu wetu waliopo ngazi ya kata.” Amesema