DAR ES SALAAM: Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa kushirikiana na Madaktari Bingwa wabobezi kutoka nchini Sudan imefanya upasuaji rekebishi kwa watu wenye macho ya makengeza.
Pia, wamefanya upasuaji wa macho kwa wagonjwa wenye changamoto ya kufunga kwa vifuniko vya macho vinavyowezesha jicho kuzunguka na kuona.
Upasuajji huo umefanyika kwenye kambi maalum ya upasuaji rekebishi wa macho ambao unahusisha watu wenye uvimbe nje ya jicho, makengeza kwa watu wazima, majeraha yatokanayo na ajali au makovu ya muda mrefu ya macho, wanaotoka machozi kwa muda mrefu kutokana na kuziba kwa njia za machozi.
Akizungumza na HabariLeo, Daktari Bingwa wa Macho wa Muhimbili Mloganzila, Catherine Makunja amesema kabla ya upasuaji huo jopo la wataalamu liliwaona na kuwafanyia uchunguzi wa awali wagonjwa wenye matatizo hayo ambao wamejitokeza kwa wingi na wamefanyia upasuaji wa macho wagonjwa wenye changamoto ya kufunga kwa vifuniko vya macho.
“Zoezi limeenda vizuri bila changamoto zozote na baadhi yao tumewaruhusu kurudi nyumbani,”amesema .
Makunja amesema kambi hiyo maalum ni ya siku tano ikishirikisha madaktari kutoka Muhimbili Upanga, Hospitali ya Benjamini Mkapa Dodoma, Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Pwani Tumbi, Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mtwara Ligula, Hospitali ya Kanda Mbeya na St. Benedict Lindi.