HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili-Mloganzila iliyopo mkoani Dar es Salaam imeanza kutoa huduma ya kupunguza uzito uliokithiri ikiwa ni hatua ya kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza.
Huduma hiyo ni kuingiza puto tumboni kupitia mdomoni hali itakayopunguza kiwango cha chakula kwa mhusika.
Hadi sasa watu watatu wenye uzito zaidi ya kilogramu 100 wamepata huduma hiyo inayogharimu kiasi cha Sh milioni 3.5 hadi milioni 4.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Profesa Mohammed Janabi alisema hawatoi huduma hiyo kwa sababu ya urembo bali wanalenga kusaidia watu.
Profesa Janabi alieleza kuwa faida kubwa ni kusaidia kukukinga na magonjwa ya kisukari, kiharusi, moyo, kushindwa kupumua.
Alibainisha kuwa matibabu yatakayotolewa ni siri ya mgonjwa ambapo pia matibabu hayo huchukua siku mbili tu.
Pamoja na hayo alisema pindi mgonjwa anapopatiwa huduma hiyo na kupungua atapata usaidizi wa mtaalamu wa lishe ili asiongeze tena kiwango cha kula na uzito kuongezeka tena.
Alisema mfumo wa bima ya afya bado haujaanza kutumika, hata hivyo alishauri watu wafanye mazoezi kukabiliana na tatizo hili.
Alisema gharama ya huduma hiyo nje ya nchi inategemea na nchi ambapo kwa India ni milioni 15 hadi 20 na Ulaya milioni 30 kwenda juu.
Alisema mwaka 2023 kwa kipindi cha Januari wanatarajia kuwahudumia wagonjwa 12 kwa gharama ya Sh milioni 3.
5 hadi 4.
Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Upasuaji, Erick Kimaro alisema wanatarajia mtu kupungua kilo 30 na kuendelea kwa muda huo wa miezi minane.
Dk Kimaro alisema kama puto likipasuka katika puto wameweka maji dawa hivyo maji yataonekana kwenye haja na itatolewa na kuwekwa nyingine.