Mmea huu dunia nzima unapatikana Kisarawe tu!

KISARAWE, PWANI:  MMEA ujulikanao kama mpugupugu uliopo katika Msitu wa Hifadhi ya Mazingira Asilia Pugu Kazimzumbwi, Wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani upo hatarini kupotea.

Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Fendey Mashimba amesema hayo alipozungumza na HabariLEO baada ya Umoja wa Uhifadhi wa Mazingira wa Kimataifa (IUCN), kufanya tathmini na kuuweka mti huo katika kundi la mimea adimu iliyo katika hatari ya kutoweka duniani.

“Hii ni aina ya mimea ambayo inapatikana katika eneo hilo tu la Pugu, kwa kitaalamu tunaita ni mimea ambayo haipatikani sehemu nyingine yoyote duniani, hata hapa Tanzania nje ya eneo hilo la Pugu Kazimzumbwi,” amesema.

 

Amesema ikishawekwa kwenye kundi la hatari ya kupotea, maana yake ni kwamba mimea iliyoko kwenye kundi la kuweza kuzaa haizidi 50.

“Kwa hiyo kwa maana nyingine kwa mujibu wa taarifa za uchunguzi uliofanyika 2011 waliuweka huo mmea katika hilo kundi kwa sababu walipoihesabu katika misitu ya Pugu Kazimzumbwi waligundua kwamba hiyo mimea haizidi 50,” amesema.

Amesema kutokana na hali hiyo, wahifadhi wanapambana kuongeza ulinzi wa hiyo misitu pamoja na mazingira yake, kuhakikisha mimea hiyo inaendelea kutunzwa kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Habari Zifananazo

Back to top button