Mmiliki Cambiasso atajwa kinara, hatari dawa za kulevya

WAKATI Kocha wa Makipa wa Simba, Mwarami Mohammed akigonga vichwa vya habari katika sakata la watuhumiwa 11 waliokamatwa na dawa za kulevya Dar es Salaam, imebainika kinara wa mtandao huo ni Kambi Zuberi Seif – mmiliki wa kituo cha kukusanya vijana na kuwaendeleza kisoka kilichoko Dar es Salaam.

Mwarami maarufu kama Shilton, Kambi na watuhumiwa wengine tisa walitangazwa mapema wiki hii na Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA).

Kwa mujibu wa Kamishna wa DCEA, Gerald Kusaya, watu hao wamekamatwa wakiwa na kilo 34.89 za dawa za kulevya aina ya heroin na biskuti 50 zilizotengenezwa kwa kutumia bangi – aina nyingine ya dawa za kulevya.

“Mwarami ni kama samaki mdogo au tuseme ni kama dagaa tu katika hili sakata hili. Unasikia bwana? Kinara hapa ni huyu Kambi Zuberi Seif. Huyu wanayemwita Mmiliki wa Kituo cha Michezo cha Cambiasso (Cambiasso Sports Academy) kilichopo Tuangoma, Dar es Salaam kinachokusanya na kuandaa vijana kwenda nje kucheza soka la kulipwa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

“Lakini haina maana Mwarami sio mtuhumiwa,” anasema mchunguzi mahiri wa DCEA aliyezungumza kwa sharti la kutotaja jina kwa sababu za kikazi.

Ofisa huyo aliyeshiriki kuwakamata watuhumiwa wote wiki iliyopita kabla ya kutangazwa wiki hii, anasema: “Huwa hatupuuzi taarifa, tumefuatilia kwa muda mrefu mtandao huu. Ni mtandao mzito. Kambi ndiye kinara, tumekusanya kila aina ya ushahidi mpaka tunawakamata na kuwatangaza hadharani.

“Yawezekana katika ripoti zetu wanahabari mmeangalia umaarufu wa Klabu ya Simba au umaarufu wa Mwarami (Mohammed Sultan), lakini mtu hatari pale ni Kambi.

“Tunafahamu kwa muda mrefu mtandao wake, haikuwa rahisi kumkamata bila ya ushahidi wa kutosha, ninavyosema ni mtu hatari katika mitandao ya dawa za kulevya, naomba unielewe,” anasisitiza.

“Achana na wake zake, huyu alimpangia apartment (sehemu ya nyumba katika jengo) mwanamke mmoja maarufu hapa mjini. Anajirusha sana instagram kule Masaki anaitwa Sanchi. Nyumba inalipwa dola 300,000 za Marekani (zaidi ya Sh milioni 6.9) kwa mwaka.

“Na alikuwa anatamba sana kwa picha mbalimbali. tazama hizi (anaonesha). Lakini nasisistiza, hili haina maana kwamba Mwarami sio mtuhumiwa, la hasha… naye yumo maana kuna mzigo umekutwa kwake na ni sehemu ya ushahidi.”

Wake watatu wa kambi akiwamo mke mkubwa, Jamila Talasisi, inaelezwa kuwa wamekimbia na vyombo husika zinafuatilia kuona kama wanahusika katika mlolongo wa watuhumiwa kwa sababu wamekuwa na mume muda mrefu, lakini walishindwa kuripoti vitendo vya jinai.

Aidha, Kambi anatajwa kushirikiana na raia wa Pakistan katika kuingiza mihadarati nchini, akipokea kati ya kilo 100 hadi 4000 kwa mwezi ndani ya mwaka.

Anatajwa kuhusika katika kesi ya mfanyabiashara maarufu wa dawa za kulevya, Fred Chonde ambaye walikamatwa pamoja mwaka 2011 wakiwa na raia wa Iran wakiwa na kilo 180 za heroin.

Wakati kesi inaendelea, Kambi akampanga Chonde ili akubali kuwa dawa ni zake ili yeye atoke kwa ahadi ya kumsaidia kutunza familia yake.

Amekuwa akianzisha biashara mbalimbali kama njia ya kutakatisha fedha haramu; biashara ya daladala na Cambiasso Sports Academy.

Novemba 15, mwaka huu, Kamishna Jenerali wa DCEA, Kusaya, mbali ya Kambi (40) na Mwarami (40), aliwatangaza watuhumiwa wengine ni Said Matwiko (41) – mkazi Magole, Maulid Mzungu maarufu Mbonde (54) mkazi wa Kisemvule ambaye ni ndugu na Mwarami.

Pia wamo John John maarufu Chipanda (40) ambaye jukumu lake kutafuta vijana wenye vipaji na kuwapeleka Cambiasso Sport Academy, Rajabu Dhahabu (32)) mkazi wa Tabata, Seleman Matola Said (24) mkazi wa Temeke Wailes, Hussein Pazi (41) mfanyabiashara na Ramadhani Chalamila (27) mkazi wa Kongowe.

Kusaya alisema pia DCEA imemkamata mfanyabiashara na mkazi wa Kaloleni Arusha, Abdulnasir Kombo (30) akiwa na biskuti pakiti 50 zilizotengenezwa kwa kutumia dawa za kulevya aina ya bangi kama moja ya malighafi akiwa anaziuza Kaloleni jijini Arusha.

Alisema katika tukio hilo la ukamataji wa biskuti zenye bangi, wamemkamata mtuhumiwa mwingine anayeitwa Hassan Ismail (25) mkazi wa Olasiti jijini Arusha anayesadikiwa kuwa ndiye mtengeneza biskuti hizo.

Alisema ukamataji huo ni mwendelezo wa operesheni zinazofanyika katika maeneo mbalimbali nchi.

“Uwepo wa bidhaa za vyakula vinavyotengenezwa kwa kutumia bangi vimeanza kushamiri hapa nchi, itakumbukwa mwaka 2020-2021 mamlaka ilikamata bangi iliyosindikwa mfano wa jam, Keki na Asali katika matukio tofauti,” alisema Kamishna Jenerali Kusaya.

Alisema tatizo hilo limeshamiri nchini hasa ikizingatiwa kuwa wafanyabiashara wenye nia ovu hutumia vyakula vinavyopendwa na watoto mfano pipi, keki, ice cream na biskuti hivyo kuwepo na uwezekano wa kuwaingiza watoto kwenye matumizi ya dawa la kulevya bila kujua na hatimaye kuwa waraibu.

Habari Zifananazo

Back to top button