Mmiliki kituo cha watoto kuendelea kushikiliwa

Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, mkoani Katavi Jamila Yusuf ameagiza kuendelea kushikiliwa na Jeshi la polisi mmiliki wa kituo cha malezi ya watoto ‘Day Care’ cha New Light Day Care kilichopo Kazima mjini Mpanda, Filbert Ferdinand.

Hatua ya kushikiliwa mmiliki huyo ni kwa uchunguzi zaidi kuhusiana na mwalimu wa kituo hicho Mussa Shaban, anayedaiwa kumfanyia ukatili wa kingono mtoto aliyekuwa katika kituo hicho.

Mmiliki wa kituo, Filbert Ferdinand. (Picha zote na Swaum Katambo).

 

DC Jamila ametoa maagizo hayo alipoiongoza Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Mpanda kwenda kutembelea na kujionea mazingira ya kituo hicho.

Akiwa kituoni hapo DC Jamila ameshuhudia mazingira yasiyoridhisha ya uendeshaji wa kituo hicho, ikiwemo kukosekana kwa vyumba maalum vya kupumzikia watoto na kutokuwa na walezi wenye sifa.

“Mazingira kama haya yanashawishi hawa watoto kufanyiwa ukatili, inaonekana hata wewe Mkurungenzi huwa huna muda wa ufuatiliaji ndio maana hili tukio lilitokea,” DC Jamila.

Pia ameagiza kufungwa mara moja kwa kituo hicho kwa kukiuka taratibu za uendeshaji, ikiwemo kuendeshwa bila usajili.

Mazingira ya kituo cha New Light Day Care kilichopo Kazima mjini Mpanda.

Katika hatua nyingine DC Jamila ameagiza Jeshi la polisi kwa kushirikiana na Idara ya Ustawi wa jamii Manispaa ya Mpanda kuwahoji watoto wote waliokuwa kituoni hapo, ili kubaini kama kuna watoto zaidi waliotendewa vitendo vya kikatili.

Habari Zifananazo

Back to top button