MWANAUME mmoja miaka 26 aliyepona ugonjwa wa Marburg, ameruhusiwa kurejea kwenye jamii.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akizungumza leo Aprili 4, 2023 jijjini Dar es Salaam amesema mgonjwa huyo ameruhusiwa baada ya afya yake kuhimarika na hakujapatikana vifo wala wagonjwa wapya.
“Jumla ya visa 8 na kati yao watu 5 wamefariki ni jambo la kumshukuru Mungu kuwa hatujapata wagonjwa wapya wala vifo ninayo furaha kubwa kuwajulisha kuwa leo tumemruhusu mgonjwa mmoja mwanaume mwenye umri wa miaka 26 akiwa na afya njema, ” amesema Ummy na kuongeza
“Ni matumaini yangu jamii itampokea na kushirikiana nae katika shughuli zake za kila siku nitoe rahi kwa jamii kutomnyanyapaa, kumpa ushirikiano wa kutosha, tumempima mara tatu tumejihakikishia hana tena ugonjwa, wasimuogope, wasimbague, ni jambo la kumshukuru Mungu kuwa hatujapata wagonjwa wapya wala vifo.”Amesema
Amesema hadi kufikia Mwezi Aprili 2023 jumla ya watu 212 walichangamana na wagonjwa 35 wamemaliza siku 21 za uangalizi bila kuonesha dalili zozote za ugonjwa huo, hivyo wameruhusiwa kuendelea na shughuli zao za kiuchumi na kuungana na familia.
Aidha, amesema wagonjwa wawili waliolazwa wanaendelea vizuri na matibabu katika vituo maalum vilivyoandaliwa hivyo serikali inatoa shukrani za pekee kwa wataalamu wote wa afya waliokuwa mstari wa mbele kutoa huduma bora kwa wagonjwa usiku na mchana kuhakikisha afya zao zinatengamaa.
Amesema serikali inaendelea kuhimiza wananchi wote na hasa wa Mkoa wa Kagera kuendelea kuchukua tahadhari kudhibiti ugonjwa na kuzuia maambukizi mpya katika Jamii na endapo kutakuwa na mtu yeyote kwenye jamii mwenye dalili za homa kali ikiwemo kutapika ,kuharisha ,kutokwa damu na mwili kuishiwa nguvu atoe taarifa haraka kwa kupiga simu 199 bila gharama zozote ili apatiwe msaada wa haraka