Mnada wa chai kuanza bila tozo

MNADA wa zao la chai nchini unaotarajiwa kuanza kufanywa jijini Dar es Salaam mwaka huu, huku serikali ikitangaza neema kwa wakulima kwamba hautakuwa na tozo.

Akifungua mkutano wa wadau wa zao la chai nchini uliofanyika mjini Iringa leo, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema uanzishwaji wa mnada huo ambao hatua zake zimekamilika, unakwenda sambamba na uanzishwaji wa maabara, maghala ya kuhifadhi zao hilo pamoja na ujenzi wa mazingira mazuri ya biashara ya majani ya chai.

“Mnada hautakuwa na tozo kwani serikali imekubali pia kuzibeba tozo hizo kwa manufaa ya taifa na wazalishaji wa zao hilo,” alisema bila kuzitaja tozo hizo.

Alisema kuanzishwa kwa mnada huo kutaongeza tija na ufanisi kwenye sekta ya chai utakaokuwa na manufaa na faida nyingi kwa wakulima wa zao hilo nchini.

Akitoa mfano alisema mnada huo utapunguza gharama za usafirishaji, utawezesha kutawala bei yake sokoni, kuongeza uwazi na uhakika wa ubora wa madaraja ya chai.

Naye Mwenyekiti wa Wadau wa Chai aliyemaliza muda wake jana, Anne Makinda alisema chai ni mojawapo ya mazao ya kimkakati hapa nchini na kwamba serikali imedhamiria kuimarisha kilimo cha zao hilo ili liendelee kuwa na tija kwa wakulima, wenye viwanda na Taifa kwa ujumla.


Kwa kupitia mkutano huo Makinda aliwataka wadau hao kusaidia kuzipatia majibu changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo na kuweka mikakati itakayozimaliza.


Awali Mkuu wa Mkoa wa Iringa Halima Dendego alizungumzia kilimo cha zao hilo mkoani kwake akisema unalima hekta 5,645 za chai katika mashamba ya wakulima wakubwa na wadogo.


Taarifa iliyotolewa kwenye mkutano huo inaonesha zao hilo kwa sasa linalimwa katika wilaya 12 katika mikoa sita ya Mbeya, Njombe, Iringa, Tanga, Kagera na Kilimanjaro huku kukiwa na hekta 23,805 zilizopandwa na kati yake hekta 12,207 ni za wakulima wakubwa na hekta 11,598 za wakulima wadogo.

Habari Zifananazo

Back to top button