MKUU wa Wilaya ya Bukoba, Moses Machali, amewatoa hofu viongozi wa serikali na wageni mbalimbali wanaowasili wilayani hapo kwa ajili ya shughuli ya kuzima Mwenge wa Uhuru, kuwa ni salama na hakuna mgonjwa wa Ebola.
Rais Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzima mwenge huo Ijumaa ya wiki hii, Oktoba 14, na viongozi mbalimbali wa serikali wa kitaifa wanatarajiwa kuanza kuwasili mkoani humo leo.
Akizungumza leo Septemba 10, 2022, Machali amesema serikali imechukua tahadhari zote muhimu na hamna kesi ya kuwapo kwa mgonjwa wa Ebola katika Wilaya ya Bukoba na Mkoa wa Kagera kwa ujumla.
“Kila siku napokea ripoti kutoka kwa waganga wakuu, mpaka sasa hatuna mgonjwa wala muhisiwa,” amesema.
Amesema pia zipo juhudi ambazo zinafanywa na serikali ikiwamo kuainisha vituo vya kuwatenga na kuwatibu wale watakaobainika kuwa na ugonjwa huo.
Pia amesema wana eneo la Nchambya, ambako ujenzi wa hospitali ya halmashauri ya Bukoba unaendelea, ambayo itatengwa maalum kwa ajili ya kutibu watu watakaobainika kuwa na ugonjwa wa Ebola na magonjwa mengine ya mlipuko.
“Wilaya ya Bukoba tumejipanga kupokea wageni wanaoingia hapa, nawahakikishia tupo salama, hakuna Ebola isipokuwa tunaendelea kuchukua tahadhari zote muhimu zinazotakiwa,” alisema Machali.

Awali Mganga Mkuu wa mkoa huo, Issessanda Kaniki, alitembelea kituo cha mabasi cha Bukoba na kutoa elimu kwa madereva wa daladala, makondakta na wapiga debe.
Kaniki aliwataka wananchi wa eneo hilo kuendelea kuchukua tahadhari wakati huu, ambao serikali inapokea wageni wengi kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya shughuli ya kuzima Mwenge wa Uhuru.
Pia alitembelea nyumba za kulala wageni na kutoa elimu hiyo pamoja na kuweka vipeperushi vitakavyosaidia kutoa elimu kwa wananchi.