DAR ES SALAAM: Sasa ni rasmi msimu ujao Klabu ya Simba itacheza Michuano ya Shirikisho barani Afrika baada ya kuzidiwa idadi ya mabao ya kufunga na Azam FC licha ya wote kuwa na pointi 69 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara iliyotamatika leo.
Licha ya Simba kushinda mabao 2-0 dhidi ya JKT Tanzania lakini haikusaidia kuwavusha kwenda Ligi ya Mabingwa baada ya Azam FC kushinda mabao 2-0 dhidi ya Geita Gold FC uwanja wa Nyankumbu.
Bao la kwanza la Simba katika mchezo huo limefungwa dakika ya 87 kwa mkwaju wa penalti na Saido Ntibazonkiza huku bao la pili kikifungwa na Willy Essomba Onana dakk ya 90, aliyeingia kuchukuwa nafasi ya Mzamiru Yassin.
Timu zote zilionyesha mpira mzuri na dakika 45 kipindi cha kwanza zilikamilika bila kufungana.
Dakika ya 30 na 31 kipa wa Simba Ayoub Lakred aliokoa mipira ya hatari iliyopigwa na David Bryson mpira wa faulo baada ya Shomari Kapombe kucheza madhambi kwa Ismael Kada. Kwa upamde wa Simba dakika 6 Luis Miquisson amekosa nafasi ya wazi alipiga shuti nje ya 18 na mpira kupaa juu ya lango.